Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imetembelea mradi wa maji wa Arusha sustainable urban water and sanitation delivery project unaotekelezwa wilayani humo ili kuona hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wake.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya amepongeza maendeleo ya mradi huo huku akiiomba Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka ya Arusha (AUWSA) kuisaidia Halmashauri ya Wilaya ya Hai kupata taarifa ya utafiti uliofanywa kuonesha ni eneo gani wanaweza kuchimba visima vya maji ili kuepuka kutumia gharama nyingine za kufanya utafiti ambao tayari ulishafanywa.
Aidha Ole Sabaya ameiomba mamlaka hiyo kuwapa pikipiki tatu watendaji wa kata unapotekelezwa mradi huo ili kusaidia katika suala la ulinzi na usalama wa vyanzo vya maji kwa kuwa fedha nyingi za serikali zitatumika hadi kukamilika kwa mradi huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Hai Yohana Sintoo amesema kuwa halmashauri yake kupitia mhandisi wa maji wilaya tayari wameshaweka makubaliano maalumu (Memorandum of understanding) na baadaye hatua zote zikikamilika itaelezwa ni jinsi gani wananchi wa Hai wanaozunguka mradi huo watakavyonufaika.
Mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya billion 476 ikiwa kiasi cha dola milioni 210.9 ni mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya maendeleo ya Afrika AFDB na kiasi cha dola za kimarekani million 22.9 ni mchango wa serikali ya Tanzania.
Kukamilika kwa mradi huo unaojulikana kama Arusha sustainable urban water and sanitation delivery project ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa maji katika jiji hilo toka wastani wa lita milioni 40 hadi kufikia lita milioni 200 kwa siku na kutoka watumiaji wa maji 325,000 hadi kufikia 600,000.
Visima 18 vitachimbwa katika wilaya ya Hai ikiwemo katika kata ya Masama Rundugai katika vijiji vya Chekimaji na Ngosero, na ukitarajiwa kukamilika mwaka 2020.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai