Serikali katika Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imeipongeza Idara ya Afya wilayani humo kwa kuvuka lengo katika zoezi la utoaji wa chanjo ya Surua Rubela lililofanywa kwa Siku wiki moja na kufanikiwa kwa asilimia 114 ikiwa ni zaidi ya lengo lililowekwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Afya ya Msingi wilaya mapema leo Ijumaa katika kikao cha mrejesho wa Kampeni shirikishi ya chanjo ya Surua na Rubela kilichofanyika katika ukumbi wa hospitali ya wilaya ya Hai kikijumuisha wajumbe mbalimbali wa kampeni hiyo.
Awali akisoma taarifa ya kampeni hiyo Mratibu wa chanjo wilaya Michael Ndowa amesema kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na msukumo na uhamasishaji wa viongozi wakuu wa wilaya wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya pamoja matangazo yaliyosambazwa kwa jamii kupitia Radio Boma Hai Fm ikitanguliwa na maandalizi ya kabla ya kampeni yaliyohusisha mafunzo kwa wasimamizi, wachanjaji na wahamasishaji.
Amesema kuwa mbali na asilimia hizo 114 kwa chanjo ya Surua na Rubela pia wamefanikiwa kutoa chanjo ya sindano ya Polio kwa asiilimia 107 na kupelekea wilaya ya Hai kuwa ya kwanza kwenye mkoa wa Kilimanjaro.
Kwa Upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai Dkt.Irine Haule amesema kuwa kampeni hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kutokana na Halmashauri kutenga bajeti ya kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 10 ambayo iliungana na bajeti ya Wizara ya afya na kusaidia kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo, amewataka watumishi wa umma katika Halmashauri yake kuendelea kuwa na ushirikiano katika utendaji wao wa kazi za kila siku za kuwahudumia wananchi ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.
Zoezi la utoaji wa chanjo ya Surua, Rubela pamoja na Polio lilifanyika kote nchini October 17 hadi 22 mwaka huu.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai