Serikali inajivunia mafanikio yanayotokana na mageuzi katika sekta ya madini yaliyopatikana ndani miaka mitatu ya mwanzo ya serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli.
Akizungumza na wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro na maeneo jirani kupitia kituo cha redio Boma Hai mapema leo Jumapili 09/12/2018 Msemaji Mkuu wa Serikali amesema kuwa serikali imefanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya madini.
Dkt. Abbas amebainisha kuwa sekta nzima ya madini nchini imeongeza makusanyo kutoka chini ya shilingi Bilioni 190 na hadi kufikia mwezi Julai 2018 mapato yamefikia shilingi billioni 301 ikiwa ni ishara ya kuongezeka kwa kiasi kikubwa mapato ya serikali ambayo ndiyo yanatumika kuwapatia wananchi huduma za elimu bila malipo na maboresho kwenye huduma mbalimbali.
Akilinganisha hali ilivyokuwa kabla ya marekebisho yaliyofanyika, Dkt. Abbas anasema kuwa mapato ya serikali kutokana na madini yalikuwa kati ya shilingi milioni 71 – 74 kwa mwaka, kwenye machimbo ya Tanzanite ambayo miezi 8 baada ya kujengwa ukuta unaodhibiti utoroshaji wa madini na kuongeza uwazi katika upatikanaji wa mapato ya serikali.
“Mererani wamepewa lengo la kukusanya shilingi billion 1.5 ambayo kwa muda wa miezi 5 hadi kufikia mwezi Novemba tayari wamefanikiwa kukusanta shilingi millioni 800 ikiwa ni zaidi ya nusu ya lengo.” Amesisitiza Dkt. Abbas.
Kwa upande wa dhahabu ya mkoani Geita, nchi ilikuwa inapoteza mapato kwenye kusafisha dhahabu ambapo mwanzo shughuli hizo zilifanyika Mwanza na hakuna aliyejua kilichopatikana.
“Serikali iliagiza kuwa mashine zote za kusafisha dhahabu ziwekwe ndani ya mkoa husika na hadi sasa zipo mashine zaidi ya 20 zinazosafisha dhahabu kukiwa na uangaliazi wa maafisa wa serikali na kufanikiwa kuongeza dhahabu kutoka kilo 70 – 160 kwa mwezi na kuongeza mapato ya serikali kwenye dhahabu kutoka millioni 400 kwa mwezi hadi zaidi ya shilingi million 900.” Ameongeza.
Aidha, Dkt. Abbas amewataka wananchi kuendelea kuiamini serikali yao na kuiunga mkono hasa wakati huu wa kutekeleza miradi mikubwa itakayobadilisha kwa kiasi kikubwa maisha ya jamii nzima ya Tanzania kwani kwa kuongeza mapato ya serikali kunaipa nguvu katika kutoa huduma bora kwa wananchi wake.
Akizungumzia maendeleo ya kufikia uchumi wa kati kwa kuwa na viwanda, Dkt. Abbas amesema kuwa hadi sasa matokeo chanya yanazidi kuonekana kwani wapo wanaonufaika na viwanda kwa kupata ajira moja kwa moja lakini pia wapo wale wanaonufaika kwa uwepo wa viwanda kwenye maeneo yao.
“takribani watanzania 26,000 wameajiriwa moja kwa moja kwenye viwanda na zaidi ya wananchi 100,000 wameweza kuanzisha biashara na kujiajiri kwa sababu ya viwanda vilivyopo” Ameongeza.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai