Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ameagiza kupatiwa eneo la ardhi Bibi Hawa Shila mkazi wa Kijiji cha Kimashuku Kata ya Mnadani wilayani Hai ili apate eneo la makazi na kufanya shughuli za kilimo .
Akitoa maelekezo ya Rais kwenye mkutano wa Kijiji hicho; Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya amesema kuwa Bibi Shila amemwandikia barua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuomba usaidizi wakuzuia kuhamishwa eneo ambalo ameishi kwa zaidi ya miaka 40 au kupatiwa eneo la makazi na kilimo ili aweze kujikimu na kuendesha maisha yake.
“Mheshimiwa Rais ameona barua yako na amenielekeza kuhakikisha kuwa unapata haki yako. Leo nimekuletea barua ya kukupa eneo la kufanya shughuli za kilimo na eneo la makazi”
Bibi Hawa Shila alifikia uamuzi wa kumwandikia barua Rais magufuli baada ya kuhamishwa kwenye eneo la mnadani lililopo kata ya Mnadani wilayani Hai ambapo ameishi kwa zaidi ya miaka 40 huku akidaiwa ameishi eneo hilo kinyume na taratibu.
“Walinifukuza nikawauliza sasa wanangu niende wapi wakasema sijui mama, eneo hilo nimemzika mume wangu na mdogo wangu hapohapo; nimezalia watoto wangu hapohapo na nimepata wajukuu hapo, basi wakaanza kunipiga vita sasa.”
Bi.Shila amemshukuru Mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya kwa kumsaidia kupata eneo hilo na zaidi akimwombea Baraka na maisha marefu Rais John Magufuli.
Baada ya maelekezo hayo Sabaya amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Hai Yohana Sintoo akishirikiana na Afisa Ardhi wilaya kusimamia umiliki wa eneo la Bibi Shila kwa kumpatia ofa na hati pamoja na kutengeneza ramani na miundombinu inayofaa kwa kuzingatia mipaka ya eneo hilo.
Eneo la ekari moja ambalo amekabidhiwa Bi.Shila linatokana na ekari tisa zilizokuwa za serikali zilizopo Kijiji cha Kimashuku Kata ya Mnadani ambazo zimegawiwa kwa kijiji hicho leo June 12, 2020 kwa ajili ya kujenga soko, zahanati na kufanya shughuli za maendeleo.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai