Serikali Yaombwa Kuongeza Majengo Kutolea Huduma Hospitali ya Wilaya Hai
Imetumwa: June 17th, 2021
Mbunge wa Jimbo la Hai Saashisha Mafuwe ameiomba serikali kutupia jicho Hospitali ya wilaya ya Hai kwa kuongeza majengo pamoja na ununuzi wa vifaa tiba ili iweze kukidhi mahitaji ya wananchi kwa kupata huduma zote muhimu.
Mafuwe ameyasema hayo mapema wiki hii wakati wa ziara yake aliyoifanya katika hospitali hiyo ambapo pia alitembelea kituo cha Radio Boma Hai Fm, pamoja na kutoa msaada kwa wananchi wenye uhitaji kisha kuhudhuria ibada ya mazishi ya aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro Mama Nsilo Swai.
Ameeleza kuwa tayari alishamuomba waziri wa TAMISEMI kuangalia hospital ya wilaya ya Hai kwa jicho la pekee kwani ndio inayohudumia wananchi wanaotoka zahanati na vituo vya Afya wilaya nzima lakini haina majengo muhimu kama jengo la Mama na mtoto, maabara huku kukiwa na uhaba wa njia zinazounganisha jengo moja na jingine.
"Kwa kweli nimuombe sana waziri, najua nimeshazungumza sana kuhusiana na hili na hata swala la gari tayari ameshalifanyia kazi, lakini kwa kweli kuna haja ya wewe kufika katika hii hospitali na kuona changamoto hizi" Amesisitiza Mafuwe.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Hai Grace Ntogwisangu amesema kuwa wanakabiliwa na ufinyu wa majengo jambo ambalo linasababisha hata wagonjwa wengine kukaa nje.
Ntogwisangu ameeleza kuwa endapo changamoto hizo zitafanyiwa kazi zitasaidie kuboresha huduma zitolewazo na hospitali hiyo katika kiwango cha juu zaidi.