Serikali katika Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imepongeza ushirikiano uliopo kati ya benki ya NMB na mamlaka za serikali za mitaa hasa halmashauri ya wilaya ya Hai.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada wenye thamani ya shilingi milioni 21 kutoka benki ya NMB; Mkuu (mshikizi) wa Wilaya ya Hai Agnes Hokororo amesema ushirikiano uliopo uendelee kuimarishwa ili kuwapatia wananchi huduma bora Zaidi.
“Niwaombe benki ya NMB, leo mmetusaidia kwenye maeneo ya afya na kilimo; niwaombe tuendelee kushirikiana kwenye maeneo haya mawili hasa kwenye zao la vanilla ambalo likipata huduma nzuri na wakulima wengi wakilima itasaidia kuongeza kipato cha wananchi ” Amesema Hokororo.
Aidha Hokororo amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya akishirikiana na Mganga Mkuu wa Wilaya kuhakikisha kuwa vifaa vilivyopokelewa vinafanya kazi iliyokusudiwa na vinasaidia kupunguza changamoto za wananchi.
Pia amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji na Mkuu wa Idara ya Kilimo wilayani Hai kutumia vizuri fedha walizopatiwa ili kuimarisha kilimo cha zao la vanilla huku akushauri uwezekano wa kuanzisha kitalu kitakachouza miche ya vanilla kwa halmashauri nyingine zinazofaa kulima zao hilo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo, ameishukuru benki ya NMB na kuahidi kutumia vizuri vifaa vilivyotolewa kwa ajili ya matumizi ya hospitali chini ya usimamizi wa Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Irene Haule lakini pia ameahidi kuzingatia matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa kuimarisha kilimo cha vanilla Mkuu wa Idara ya Kilimo David Lekei.
Kwa upande wake Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini Aikansia Muro amesema benki ya NMB imejiwekea utaratibu wa kurudisha kwa jamii faida wanayoipata na kwa sasa wamijizatiti kumuunga mkono Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusaidia shughuli za huduma ya jamii hasa elimu na afya huku akimhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa wataendelea kushirikiana na halmashauri ya Wilaya ya Hai kuboresha huduma kwa jamii.
Awali akisoma taarifa ya shughuli za kuimarisha zao hilo; Mratibu wa zao la Vanilla wilaya ya Hai Simon Gunda amesema kuwa fedha zilizotolewa na NMB zitatumika kuwafikia Zaidi ya wakulima 1,200 kwenye vijiji 43 katika kata 10 ambapo kila kijiji watachaguliwa wakulima 30 watakaopewa mafunzo ya zao hilo na watauziwa miche kwa bei ya ruzuku ambayo itanunuliwa kutokana na sehemu ya fedha iliyotolewa na benki ya NMB.
Benki ya NMB imetoa msaada wenye thamani ya shilingi miliani 21 kwa kutoa vitanda vinne vya kupumzikia wagonjwa na vitanda viwili kwa ajili ya kujifungulia lakini pia kutoa shilingi milioni 16 kwa ajili ya kuimarisha zao la vanilla.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai