Serikali kupitia wizara ya elimu imetangaza utaratibu mpya kuwa wanafunzi watakaolala katika shule za bweni utaanzia darasa la tano na kuendelea na kufuta utaratibu wa awali ulikuwa ukiruhusu watoto chini ya darasa la tano kulala katika shule za bweni kufuatia mmomonyoko wa maadili unaosababishwa na utandawazi.
Akizungumza na waratibu elimu kata kwenye kikao kilichofanyika Januari 20, 2023 katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Hai, mdhibiti ubora wa shule wilaya hiyo ameeleza kuwa wizara ya elimu imetangaza mabadiliko kwa mujibu wa sera, taratibu na kanuni za miongozo.
“kuna wanafunzi wanalala kwenye shule za bweni kuanzia darasa la awali, mwanzo ilikuwa inaruhusiwa lakini kutokana na mambo yalivyokuwa mabaya mabaya sasaivi, utandawazi wizara imebadilisha kwamba wanafunzi kulala bweni ni kuanzia darasa la tano na siyo vinginevyo”
“lakini pia kuna baadhi ya shule za Sekondari ambazo ambazo shule zikifungwa zinawanyima wanafunzi kwenda likizo mpaka krismasi wanalia kule shuleni, wanapikiwa pilau safi, wanafunzi wanafurahi lakini watoto wanatakiwa wapumzike, tunazitaka hizo shule tupewe majina yao na tunazifahamu”
Pia amegusia suala la wanafunzi kubebeshwa mabegi mazito yenye madaftari makubwa (counter book) hali inayopelekea watoto kulemewa hadi kuota kibiongo hivyo ametumia nafasi hiyo kuwaelekeza walimu pamoja na wazazi kuhakikisha kuwa watoto wanabeba mabegi yenye madaftari madogo yasiyowaelemea.
Mkuu wa divisheni ya elimu sekondari wilaya ya Hai Julius Mduma amewataka waratibu elimu kata waliosaini mikataba hiyo kwenda kuisimamia ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miongozo ya elimu iliyomo katika mikataba hiyo na inakataza baadhi ya mambo ikiwemo katazo la watoto wadogo kulala bweni, inatekelezwa na shule zote bila kukiukwa.
Afisa tawala wilaya ya Hai Mary Mnyawi, akimwakilisha mkuu wa wilaya hiyo Juma Irando, ameeleza kuwa kwa sasa serikali imeamua kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu hivyo kuwataka watendaji waliopo katika sekta hiyo kuwajibika kikamilifu ili kuendana na mabadiliko hayo hali itakayosaidia kuleta matokeo chanya.
Mkuu wa idara ya utumishi wilaya ya Hai Suzan Nyanda amewataka waratibu wa elimu kata kuhakikisha kuwa kila mtumishi (mwalimu) anaishi karibu na eneo lake la kazi na kuacha kukimbilia kuishi mjini ambapo ni mbali na eneo la kazi lengo likiwa ni kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai