SHIRIKA la Nyumba nchini(NHC) limesema litaendelea kutekeleza miradi mbalimbali inayokabidhiwa na Serikali Kuu huku likizingatia viwango vinavyokubalika kitaalam.
Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Dkt. Maulid Banyani, wakati wa hafla ya kukabidhi jengo jipya la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, iliyofanyika wilayani humo mwishoni mwa wiki.
“Tunaishukuru Serikali, hususan ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kuendelea kuiamini NHC na kuipa miradi mbalimbali ambapo kwa sasa kuna miradi zaidi ya 40 ambayo inatekelezwa na NHC hapa nchini”, amesema.
Alisema NHC kuendelea kuaminiwa na Serikali na kupewa miradi hiyo ni kazi nzuri ambazo zimekuwa zikifanywa na shirika hilo wakati wa kutekeleza miradi mbalimbali ambapo alisema shirika hilo litaendelea kufanya kazi kwa weledi. .
Aidha amempongeza Rais Dkt.Magufuli kwa kuwa na maono yaliyopelekea Watanzania kuendelea kufanya kazi huku wakichukua tahadhari wakati Dunia ikiendelea kupambana na ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya Corona.
“Kama tungelazimishwa kujifungia ndani kama mojawapo ya tahadhari ya kuepusha maambukizi mapya ya virusi vya Corona hata mradi huu usingeweza kukamilika kwa wakati uliowekwa na hapa ndipo umuhimu wa maono mazuri aliyokuwa nayo Rais wetu unapoonekana”, Ameongeza Dkt. Banyani.
Akitoa ripoti ya mradi huo,Yusuph Bigambo kutoka wakala wa Majengo Tanzania (TBA), taasisi hiyo ilisanifu na kusimamia mradi huo kama Mshauri Elekezi Mkuu kwa ushirikiano na Mshauri Elekezi Msaidizi upande wa Umeme na Mitambo.
“Mradi huu ambao umetekelezwa na NHC kama Mkandarasi Mkuu ulianza rasmi Mei, 2019 na kukamilika Mei, 2020; mpaka sasa umegharimu jumla ya shilingi 1,092,327,322.92”, alisema.
Akizungumza kwa niaba ya KatibuTawala Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Dkt. Hatib Kazungu, Katibu Tawala Msaidizi Sekretarieti ya Mkoa wa Kilimanjaro Bi Lyidia Riwa amelipongeza Shirika la Nyumba kwa kukamilisha mradi huo kwa muda na ubora uliotarajiwa.
“Nitoe rai kwa uongozi wa Serikali wilaya ya Hai kuhakikisha jengo hili linatunzwa vyema ili liweze kudumu kutokana na kuwa Serikali imetumia pesa nyingi katika kutekeleza mradi huu hii ikiwa ni sehemu ya ahadi ya Rais Dkt. Magufuli ya kuweko na ofisi bora nchini kote”, alisema.
Akitoa shukrani kwa niaba ya uongozi wa wilaya ya Hai, Katibu Tawala wa wilaya hiyo Upendo Wela, ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha zilizowezesha ujenzi wa jengo ambapo amesema miundombinu bora hiyo itakuwa chachu ya viongozi wa Serikali ya wilaya hiyo kuongeza ufanisi wa utendaji wake hasa katika kuwahudumia wananchi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai