Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hai Elia Sintoo ameipongeza shule ya sekondari Harambee kwa matokeo mazuri waliyoyapata wanafunzi wa kidato cha sita katika shule hiyo ikiwa ni pamoja na kushika nafasi ya tano katika mkoa wa Kilimanjaro kwa matokeo ya mtihani wa Mock.
Akizungumza ofisini kwake wakati wa kuwatunuku zawadi wanafunzi waliofanya vizuri, Sintoo amessema kuwa matokeo hayo yameitia moyo halmashauri yake na kama wasimamizi wakuu na hivyo kuamua kuwapongeza kwa kuwapa kiasi cha fedha taslimu shilingi elfu hamsini na kusema kuwa matamanio ni kuona shule hiyo ikifanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa mwisho wa kidato cha sita.
Aidha pia amebainisha kuwa kwa nafasi iliyoshika shule hiyo halmashauri yake inatarajia kuona shule hiyo ikiwa kinara katika nchi kwenye viwango vya ufaulu na kuwataka waalimu na wanafunzi kuendelea kushirikiana ili kuinua kiwango cha ufaulu.
Kwa upande wao wanafunzi walioongoza katika nafasi ya kwanza hadi ya tatu ambao ni Jcline Verande Ahirikyamuu, Lilian James Sichula pamoja na Magreth Godwin Nyamwela wamemshukuru Mkurugenzi mtendaji kwa kuamua kuwapa motisha ya zawadi kwani itasaidia kuwapa hari ya kusonga mbele huku wakieleza kuwa chanzo cha mafanikio hayo ni nidhamu na utii kwa waalimu pamoja na viongozi wao.
Naye mkuu wa shule hiyo Mwalimu Florence Thomas Muhochi amewaomba waalimu na wakuu wa shule nyingine kuzibadili changamoto kuwa fursa na kuzitumia ipasavyo mbali na kuishia kulalamika huku pia akiahidi shule yake kuitoa halmashauri kimasomaso katika matokeo ya kidato cha sita.
Ikumbukwe kuwa shule ya Harambee ilianzishwa mwaka 2003 kwa nguvu za wananchi wa kata ya machame kaskazini kwa kidato cha kwanza hadi cha nne na badae mwaka 2017 ikapata kibali cha kuanzisha kidato cha tano na sita
Katika matokeo ya mtihani wa Mock kwa mwaka huu shule ya Harambee haikuwa na waliofeli (division zero) wala daraja la nne (division four) ambapo kwa mwaka huu itatoa wanafunzi wa kidato cha sita kwa mara ya kwanza na idadi yao ikiwa ni wanafunzi 51.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai