Wananchi wa Kata za Masama Rundugai na Machame Mashariki wametakiwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya BOOST iliyotambulishwa na halmashauri ya wilaya ya Hai ili kuhakikisha miradi hiyo inaleta matokeo chanya kwa jamii.
Kauli hiyo imetolewa Julai 21, 2025 na kaimu Afisa Elimu Msingi wa wilaya ya Hai Jafari Zaidi wakati wa utambulisho rasmi wa miradi hiyo kwa wananchi wa kata husika.
Zaidi amesema serikali tayari imetoa shilingi milioni 63.6 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika Shule ya Msingi Rundugai, ambapo kutajengwa madarasa mawili ya elimu maalum pamoja na matundu sita ya vyoo na kwamba shule ya msingi Nkweshoo imepatiwa zaidi ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya ukarabati.
“Leo tumetambulisha miradi ya BOOST ambapo awali tulipokea bilioni 1.5 lakini kwa siku ya leo tumetambulisha shule mbili ambapo shule moja ni shule ya msingi Rundugai wao wamepokea jumla ya shilingi milioni 63 na laki sita,kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili ya elimu maalum na matundu sita ya vyoo,lakini pia tumetambulisha mradi mwingine katika shule ya msingi Nkweshoo wao wamepokea milioni 100 na 1 kwa lengo la kufanya ukarabati wa shule nzima, tumezungumza na wananchi tumewasihi wajitolee nguvu kazi na wamekubali”Amesema Jafar Zaidi.
Kwa upande wake kaimu afisa mazingira wa wilaya ya Hai Lightness Urassa, amezitaka kamati zitakazosimamia miradi hiyo kuzingatia utunzaji wa mazingira wakati wote wa utekelezaji wa miradi ili kuepusha athari zinazoweza kuwapata wanafunzi na jamii kwa ujumla.
“Ningependa kuzungumzia kuhusu zile zana tutakazo zitumia katika ujenzi wetu,najua kutakuwa na vibao bao,kutakuwa na misumari na mifuko ya saruji,hawa malaika wanaweza wakawa rafiki wa vile vitu kwani watapenda wavichezee,wao wanapenda michezo lakini ni hatarishi kwao kwa hiyo ninaomba sana zana hizi zisichafue mazingira”Amesema Urassa.
Wananchi waliojitokeza kwa ajili ya kupokea miradi hiyo wameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za miradi hiyo, huku wakiahidi kushiriki kikamilifu kwa kutoa mchango wa nguvu kazi hadi miradi ikamilike.
Kwa ujumla, halmashauri ya wilaya ya Hai imetambulisha jumla ya miradi 13 chini ya mpango wa BOOST, ambayo inakadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni moja, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha miundombinu ya elimu nchini.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai