Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais –Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa David Silinde (MB) amewataka wananchi kuondoa hofu zinazosababishwa na taarifa za uongo zinazosambazwa dhidi ya ugonjwa wa Corona ila wachukue tahadhali za msingi zitakazoimarisha afya zao.
Ameyasema hayo leo Februari 11 wakati wa ufunguzi wa jengo la huduma za kinywa na meno katika hospitali ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro lililojengwa kutokana na fedha za makusanyo ya mapato ya ndani.
Ameitaka jamii kuzingatia maelekezo ya Serikali hasa yanayotolewa na Rais John Magufuli kuwa ugonjwa wa Corona unatibika kwa nguvu za Mwenyezi Mungu na kutumia dawa lishe kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya.
Aidha Naibu Waziri Silinde amezitaka halmashauri nyingine nchini kuiga mfano wa halmashauri ya Hai kwa kutekeleza miradi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi kwa kutumia vyanzo vya fedha za mapato ya ndani badala ya kusubiri kila kitu kifanywe na serikali kuu.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya ametumia uzinduzi huo kuwatoa hofu wananchi kuhusu maambukizi ya ugonjwa wa Corona kwa kuwataka wasiogope kufanya shughuli zao za maendeleo kama ilivyo desturi na kujitafutia kipato chao na familia zao kwa kuwa hofu ndio inayokatisha maisha yao.
Amesema kumekuwepo dhana yenye mitazamo tofauti juu ya kila anayefariki dunia kuelezwa kuwa amekufa kwa ugonjwa huo jambo hilo linasababisha wananchi kujawa na hofu na wengi wao kupoteza maisha na kusisitiza kuwa wilaya hiyo ipo salama.
Hata hivyo Sabaya amewataka wananchi kuendelea kuchukua hatua za kujikinga kwa kujifukiza majani yaliyoletwa na Mungu na kufanywa dawa ya kuwaponya na kuepuka matumizi ya chanjo ambayo ni biashara ya mabeberu na si salama sana.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dkt Irene Haule amesema Jengo hilo la huduma za kinywa na meno limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 82 fedha ambazo zimetokana na mapato ya ndani.
Hata hivyo amesema kumekuwepo na changamoto ya upungufu kwa watumishi katika idara ya afya wilayani humo hasa katika kitengo cha huduma ya kinywa na meno kwani kati ya watumishi 10 wanaohitajika kwa sasa kuna watumishi watatu tu jambo ambalo linaleta changamoto kubwa katika utoaji huduma ya kinywa na meno kwa ufanisi.
Jengo la kinywa na meno katika hospitali ya wilaya ya Hai limegharimu kiasi cha shilingi milioni 82 hadi kukamilika kwake likitegemewa kuleta mapinduzi makubwa kwenye huduma mbalimbali za kinywa na meno ambazo awalii hazikuweza kufanywa kwenye hospitali hiyo kwa sababu ya kukosa vifaa.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai