Skimu ya Umwagiliaji iliyogharimu zaidi ya Mil 900 yaathiriwa na Mafuriko.
Imetumwa: April 25th, 2021
Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe ametembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko wilayani Hai ikiwa ni pamoja na kutoa mkono wa pole kwa Wananchi walioathiriwa na mafuriko hayo.
Mapema hii Leo Saashisha alitembelea kata ya Weruweru kujionea athari za mafuriko hayo huku pia akiwaomba wananchi kuwa watulivu wakati serikali ikiendelea na taratibu za kulishughulikia tatizo hilo.
Saashisha amesema kuwa baada ya kutembelea eneo hilo amebaini kuwa wizara ya kilimo kupitia Waziri wake Prof Adolf Mkenda (Mb) inapaswa kufika katika kata hiyo ambayo kwa asilimia zaidi ya 78 wananchi wake wanategemea kilimo ambapo kwa sasa Skimu kubwa ya umwagiliaji iliyopo katika kata hiyo iliharibiwa na mafuriko.
"Nimuombe waziri wa kilimo Prof. Mkenda kwa kushirikiana na wataalamu wa wizara yake waje Hai wajionee, Skimu hii iliigharimu serikali kiasi cha zaidi ya shilingi Milion 900 na ni uwekezaji mkubwa mno."
"Kata hii ya Weruweru inategemea sana kilimo cha umwagiliaji, kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa tutasababisha maafa mengine zaidi." Alisema Saashisha.
Mbali na uharibifu wa Skimu hiyo ya umwagiliaji wapo wananchi walioachwa bila makazi baada ya nyumba zao kubomolewa na maji ambapo mbunge Saashisha alitoa mkono wa pole kwa kuwapatia vitu mbalimbali vya kujikimu ikiwemo Unga, Sukari na Magodoro ambapo pia taratibu nyingine za kushughulikia majanga ya maafa chini ya kamati ya maafa wilaya zikiwa zinaendelea.
Mbali na kata hiyo ya weruweru, pia athari hizo za mafuriko ziliikumba kata ya Masama Mashariki baada ya mto Namwi kufurika na kuleta uharibifu mkubwa ikiwemo kuharibu nyumba na mashamba.
Ikumbukwe kuwa mafuriko hayo yalitokea usiku wa kuamkia tarehe 22 mwezi April ambapo pia wananchi watatu wa kata hiyo hawajulikani walipo licha ya ghari wapilokuwa wakisafiria kukutwa limezama ndani ya Mto Namwi na kuchukua zaidi ya siku moja kulinasua katika eneo hilo.
Hii leo pia ulipatikana mwili mmoja huku wananchi wa kata hiyo wakiaswa kwenda kuutambua kubaini kama ni miongoni mwa vijana hao huku baadhi ya wananchi wakisikika wakisema kuwa kwa ziaid ya miaka 40 hawajawahi kushughudia tukio kama hilo.