Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mwita Waitara amewataka watumishi na viongozi katika Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuimarisha maendeleo ya wananchi kama inavyoelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi inayosimamia serikali.
Akizungumza kwenye mkutano na watumishi wa wilaya hiyo, Naibu Waziri Waitara amesema kuwa Wizara ya TAMISEMI inaunga mkono juhudi zinazochukuliwa na viongozi hususan Mkuu wa Wilaya hiyo Lengai Ole Sabaya zikiwa na juhudi za kuboresha maisha ya wakazi wa wilaya.
“Endeleeni kutafuta haki za wananchi waliodhulumiwa; wale walioguswa wakija kwetu tutaangalia kama mmewaonea, lakini kama mmesimamia haki sisi kama TAMISEMI tutawaunga mkono”. Amesema.
Aidha amewashauri viongozi na watumishi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na taratibu husika bila kupendelea wala kumuonea mtu yeyote.
Awali akitoa tathmini ya kazi, Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya amemweleza Naibu Waziri wa TAMISEMI kuwa wilaya inaendelea kutatua changamoto za wananchi kwenye masuala ya ardhi, ushirika na aina nyingine za madhila ikiwemo kuondoa matabaka miongoni mwa wananchi.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai Dkt. Irene Haule amesema kwa kushirikiana na vyama vya ushirika wilaya imeanza ujenzi wa kituo cha afya kwenye Kijiji cha Longoi kitakachohudumia wakazi wa kata za Masama Rundugai, Weruweru na Mnadani zenye Zaidi ya wakazi 30,000 kikitoa huduma zote za kawaida na dharura.
Kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wameonesha kufurahia wazo la kupata kituo cha afya kwenye maeneo yao ambacho kitawapunguzia adha ya kwenda umbali mrefu kupata huduma huku wakiahidi kuwa tayari kushirikiana na serikali kwa kuchangia nguvukazi ili kukamilisha ujenzi wa kituo hicho.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mwita Waitara amefanya ziara ya kikazi ya siku moja kwenye wilaya ya Hai ambapo amepata wasaa wa kuzungumza na watumishi wa Wilaya hiyo wakiwemo wakuu wa shule za sekondari, waratibu wa elimu ngazi ya kata, watendaji wa vijiji na kata pamoja na wakuu wa idara na vitengo pamoja na watumishi wa makao makuu ya halmashauri.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai