Wito umetolewa kwa wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai wakiwemo Wakuu wa Idara na wawezeshaji kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu ili kutimiza malengo yaliyowekwa na Serikali katika kuhudumia wananchi wake.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kwa wakuu wa idara za halmashauri na wawezeshaji wa TASAF ngazi ya wilaya; Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amewataka watumishi wa Umma wanaoshiriki mafunzo hayo kuwa wasikivu ili ujuzi watakaoupata ukawasaidie kufanikisha malengo ya Serikali.
“Niwaombe ndugu zangu mnaopata mafunzo haya; kujifunza kwa umakini mkubwa na kwenda kutumia ujuzi mtakaoupata hapa kwa weledi na uaminifu mkubwa mkiweka mbele maslahi ya Taifa na huduma kwa wananchi wetu” Ameongeza Sintoo.
Akitoa hotuba ya ufunguzi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAF Ladislaus Mwamanga; Makwinja Dismas amesema kuwa mafunzo watakayoyapata yamelenga kuwaongezea ujuzi wataalamu katika kutambua na kutoa taarifa sahihi za wanufaika wa miradi ya TASAF katika wilaya.
Amesema zoezi la kutambua walengwa linafanyika kwa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli wakati wa kuzindua awamu ya pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini huku akibainisha kuwa kumekuwa na taarifa za malalamiko kuwa wapo wanufaika ambao hawastahili kunufaika na mpango huo huku wakiwepo wenye uhitaji ambao hawajapata nafasi kwenye mpango huo.
Amesema kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF inategemea kuwafikia wanufaika Zaidi ya milioni 7 kwenye kaya milioni moja laki nne na nusu ikiwa ni nyongeza ya kaya laki tatu na nusu huku akibainisha kuwa awamu hii inaweka mkazo kwa kaya kufanya kazi ili kuongeza kipato.
Aidha Makwinja amekumbusha kuwa ni jukumu la kila mmoja kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona kama inavyoelekezwa na Wizara ya Afya kuhusu kunawa mikono kwa maji na sabuni, kuepuka misongamano pamoja na kukaa umbali wa mita mbili kati ya mtu mmoja na mwingine.
Kikao kazi hiki kinalengo la kuwaandaa wawezeshaji wa TASAF wa halmashauri ya wilaya ya Hai ikiwa ni maandalizi ya zoezi la uhakiki wa kaya zinazonufaika na Mradi wa Kunusuru Kaya Masikini.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai