Serikali katika Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imewataka watumishi walioaminiwa kushiriki kazi za TASAF wilayani humo kufanya kazi kwa uadilifu ili kufanikisha lengo la mfuko huo katika kuondoa umasikini kwenye jamii.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha watendaji wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Kunusuru kaya masikini katika ukumbi wa halmashauri ya Wilaya ya Hai mapema leo 10/08/2021, Mkuu wa Wilaya hiyo Juma Irando amewataka watendaji hao kuwa wavumilivu na mabalozi wazuri wa mfuko huo.
Irando amewaasa wanasiasa kuepuka kujiingiza katika mchakato wa kuwapata walengwa kwa kuingiza watu wasiostahili kwa vigezo vya upendeleo bali wawasaidie wataalamu kusimamia miongozo iliyowekwa kuwatambua walengwa.
“Vigezo na masharti vizingatiwe katika kutekeleza kazi za TASAF Kipindi cha Awamu ya Tatu. Tusiweke siasa na upendeleo”. Amesema Irando.
Aidha Irando amewataka watendaji kutumia muda kutoa elimu sahihi kwa wananchi kwani kwa uelewa sahihi jamii itapunguza manung’uniko yasiyo ya lazima.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Hai Wang’uba Maganda amewataka watendaji kuwa waaminifu katika majukumu wanayokwenda kutekeleza.
Maganda ameongeza kusema kuwa iwapo watendaji wakitekeleza wajibu wao vizuri ndipo sehemu ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi inayohusu kuimarisha wananchi kiuchumi itakuwa imetekelezwa.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Swalehe Swai ameshukuru utaratibu wa kuwashirikisha madiwani katika masuala ya TASAF kwani wao ndiyo wanaokaa na watu kwenye jamii hivyo ni rahisi kutambua wananchi wa maeneo yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Dionis Myinga ametumia kikao hicho kujitambulisha kwa watumishi na viongozi waliokuwepo kwani ni mara yake ya kwanza kushiriki matukio ya kijamii tangu alipokabidhiwa ofisi tarehe 09/08/2021.
Amewaomba watumishi na viongozi kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yaliyo mbele yake na zaidi katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Wilaya ya Hai.
Kikao kazi hiki kilichoongozwa na Caroline Kimaro Afisa Ufuatiliaji anayemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF kinafanyika kwa siku moja ili kuwaandaa watumishi watakaofanya kazi ya kuwezesha shughuli za TASAF katika Wilaya ya Hai.