Mbunge wa Jimbo la Hai Mhe. Saashisha Mafuwe amewahakikishia wananchi katika wilaya hiyo kuwa Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuboresha maisha yao katika kipindi cha miaka mitano ya 2020 hadi 2025.
Akizungumza kwenye kikao na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai mapema leo Jumatatu Novemba 30, 2020 Mafuwe amesema kuwa viongozi na watumishi wa umma wapo kwenye nafasi zao ili kuwatumikia wananchi.
“Wananchi wa Wilaya ya Hai ndiyo mabosi na waajiri wetu. Mimi Mbunge, Mkurugenzi na watumishi wote tunao wajibu wa kuwatumikia wananchi na kuhakikisha tunaboresha maisha yao”
“Sisi tuliopo humu ndiyo wenye jukumu la kujibu matarajio ya wananchi wa Hai ambao wanaonesha Imani kubwa kuwa jimbo hili sasa linaenda kubadilika” Amesema.
Mafuwe amesema kuwa kazi yake ya kwanza ni kushirikiana na halmashauri kuongeza mapato kwa kubuni vyanzo vipya na kuimarisha yanzo vilivyopo akiamini kuwa serikali yenye pesa inaweza kutoa huduma kwa uhakika.
“Tutafute mapato ili tuweze kutoa huduma kwa wananchi kwenye jimbo na wilaya yetu. Serikali yenye fedha inaweza kutoa huduma za elimu, afya, barabara na nyinginezo kwa uhakika na ufanisi zaidi” Amesisitiza Mafuwe
Aidha, Mafuwe amesema atashirikiana kwa karibu na watumishi wa halmashauri kila mmoja kwa eneo lake la ubobezi ili kutoa huduma sahihi na ya kuridhisha kwa wananchi.
Amewataka wataalamu hao wa halmashauri kuwa tayari kutumia taaluma zao kwenye kutekeleza vipaumbele vya kuifanya Wilaya ya Hai kuwa ya uchumi wa kilimo na viwanda.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amemuhakikishia Mbunge Mafuwe kuwa ofisi yake na idara zote za halmashauri ziko tayari kufanya kazi kwa kushirikiana na mbunge kufanikisha lengo kuu la kuwahudumia wananchi wa jimbo la Hai.
Mbunge wa Jimbo la Hai Mhe. Saashisha Mafuwe amefanya kikao na watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Hai ikiwa ni sehemu ya kujitambulisha kwao na kuweka mikakati ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi katika kuwahudumia wananchi wa jimbo la Hai.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai