Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Hai na diwani wa kata ya Muungano Edmund Rutaraka ameitaka kamati ya shule ya msingi Mlimashabaha kutumia shilingi milioni 12.5 kutekeleza miradi iliyokusudiwa ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Rutaraka ameyasema hayo wakati wa ziara yake kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea katika kata hiyo.
Ameongeza kuwa fedha hizo zimetengwa na Halmashauri ya wilaya ya Hai kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na kwamba tayari zimeingizwa katika akaunti ya shule hiyo ambapo darasa moja limefikia katika hatua ya kupaua.
"Serikali kupitia Halmashauri yetu ya wilaya ya Hai imeweka milioni 12.5 kwa ajili ya kumalizia hayo madarasa" amesema Rutaraka.
"Hela ipo kwenye akaunti ya shule tayari na mmeshaanza kuitumia katika ujenzi huo hivyo kamati ya shule hakikisheni mnaitumia kwa malengo yaliyokusudiwa kikamilifu" Ameongeza.
Aidha katika ziara hiyo Mwenyekiti Rutaraka ametembelea shule ya sekondari ya kutwa na bweni Hai na kueleza kuwa serikali imepanga kupeleka shilingi Milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 18 ya vyoo shuleni hapo kwani kwa sasa matundu yanayotumika ni 6 pekee kwa wanafunzi zaidi ya 1200 wa shule hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo Alex Warioba ameeleza kufurahishwa na ziara ya mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa ujio huo unakwenda kuzaa matunda ya kukamilika kwa miradi ya ujenzi inayoendelea katika shule hiyo kwa muda uliopangwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka amejiwekea utaratibu wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye miradi inayotekelezwa kwenye kata yake lakini pia kwenye kata zote za Halmashauri ya Wilaya ya Hai.