Serikali katika Wilaya ya Hai yazindua mpango maalumu wa kuimarisha ulinzi wa mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji ikiwemo mimba za utotoni, ubakaji na ulawiti.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya kumlinda mtoto; Mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya amesema kuwa ofisi yake pamoja na ofizi zilizo chini yake zina jukumu la kuhakikisha kuwa mtoto anakuwa salama; uzinduzi ambao ulitanguliwa na maandamano ya Amani kutoka ofisi za halmashauri ya Wilaya ya Hai hadi kwenye viwanja vya Snow view yaliyoongozwa na bendi ya Polisi na kuhudhuriwa na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, walimu, wazazi.
“Watumishi wote wa Serikali wana kazi ya kwanza ya kuwalinda watoto dhidi yetu sisi ‘wanaume’ tunaowaka tamaa ambao kila sketi ikipita mbele yetu tunaona ni haki yetu”
Akizungumza kuhusu kampeni ya kumlinda mtoto; Sabaya ameiagiza kamati kamati ya ulinzi wa mtoto kuhakikisha kuwa elimu kuhusu ulinzi wa mtoto inamfikia kila mwananchi katika wilaya ili pale hatua zitakapochukuliwa kuwe na uelewa wa pamoja.
“Mimi ndio niliwapa kazi hii kwa niaba ya Serikali ya Wilaya ya Hai, sasa leo nawaongezea kazi. Nawatafutia shilingi milioni 10 ili mwende kwenye shule zote za wilaya hii mkawapatie elimu hii” Aliongeza Sabaya.
Aidha Sabaya ameviagiza vyombo vya dola ikiwemo TAKUKURU kuwakamata wale wote watakaohusika na mashauri ya usuluhishi inapotokea mtoto amepewa ujauzito na kwamba wote watakaohusika na usuluhishi wajumuishwe kwenye kesi ya ubakaji ili kuondokana na tabia ya jamii kumaliza kirafiki kesi za unyanyasaji kwa watoto,
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi wa mtoto ya wilaya ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Hai Upendo Wella ameahidi kuzihuisha kamati za ulinzi wa mtoto ngazi ya kata na vijiji ili kuimarisha ulinzi wa mtoto katika wilaya ya Hai.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya Irine Haule ametaja madhara yanayopatikana kwa mtoto kushiriki ngono akiwa kwenye umri mdogo kuwa ni pamoja na maambukizi ya magonjwa, uharibifu kwenye mfumo wa uzazi na kuitaka jamii kuepusha watoto na vitendo vya ngono.
Akiwageukia wazazi kama sehemu kuu ya ulinzi wa mtoto Afisa Ustawi wa Jamii Helga Simon amewataka wazazi kuonesha upendo kwa watoto wao ikiwa ni pamoja na kuwapa nafasi ya kuwasikiliza ili kufahamu maendeleo yao lakini pia kusikia changamoto wanazokutana nazo na Zaidi kuwazoesha watoto kujieleza wanapokutana na changamoto kwani watoto wakikosa upendo nyumbani watautafuta mitaani kwa watu wasio sahihi hivyo kuingia matatani.
Mkuu wa Wilaya aliamua kuunda kamati hii maalumu kwa lengo la kupambana na aina zote za ukatili kwa watoto baada ya kuona kiwango cha matukio ya ukatili na unyanyasaji kwa watoto yanaongezeka ikiwemo mimba za utotoni zilizoongezeka kutoka 26 mwaka 2018 hadi 36 mwaka 2019 huku akiipa kazi kamati kutoa elimu kuhusu masuala ya ukatili na unyanyasaji ya watoto na aina zake lakini pia kushirikiana na wadau wote wanaohusika kuhakikisha kuwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kufanya ukatili au udahilishaji kwa mtoto anapatiwa adhabu stahiki.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai