Wananchi wa kata ya Mnadani Wilayani Hai wameipongeza serikali kwa kutoa fedha shilingi Millioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Shirimatunda
Waliyasema hayo wakati wakishiriki kuchimba msingi kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa shuleni hapo wakishirikiana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za serikali, ambapo walisema mpango wa serikali kutoa fedha hizo umelenga kuwawezesha watoto kusoma katika mazingira rafiki.
Diwani wa kata ya Mnadani Nasib Mndeme aliwapongeza wananchi wa kata hiyo kwa kujitokeza ambapo amewaomba kuendelea na ushirikiano ili kuipeleka haraka shughuli hiyo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa
Mndeme ameihakikishia serikali kuwa pesa hiyo waliyopatiwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ataisimamia vizuri ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kukamilika kikamilifu
Kwa upande wake Magreth Matiliya kutoka kijiji cha Shirimatunda ,amesema Ukosefu wa shule ya sekondari katika kata hiyo imekuwa changamoto kwa wanafunzi wa kata hiyo hali inayowalazimu wanafunzi kutembea umbali wa kilomita 8 hadi sekondari ya Mailisita huku wengine wakilazimika kwenda kata ya Weruweru kwa ajili ya masomo.
Alex Utaro, ni miongoni mwa wakazi wa kata hiyo amesema kuwa wanafunzi wote wanaochaguliwa kujiunga na sekondari katika kata hiyo wanalazimika kuondoka saa kumi alfajir kwenda kata jirani ambapo kuna shule ya sekondari jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Dionis Myinga alisema halmashauri hiyo imepokea fedha kutoka serikali kuu chini ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na UVIKO 19 ,ambazo zimelenga kuwezesha wanafunzi wote wa kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2022 kujiunga na kidato cha kwanza kwa wakati mmoja,badala ya awamu mbili.
Edmund Rutaraka ambae pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai amesema ujenzi wa shule ya sekondari Shirimatunda umegharimu nguvu za wananchi na Serikali ambapo aliwaomba wananchi kuendela kuchangia mali na nguvu zao kwenye miradi ya maendeleo.
Hata hivyo mkuu wa Wilaya hiyo , Juma Irando aliwaomba wananchi kuwa tayari kuchangia miradi ya maendeleo wakati miradi inapo anzishwa ili kuondoa changamoto zinazo wakabili wananchi na kuondokana na kutembea umbali mrefu kufuata elimu kata ya jirani pamoja na huduma za afya
Kata ya mnadani ina shule moja ya sekondari na Shule kumi za Msingi ambapo kati ya hizo sita ni za serikali na nne zinamilikiwa na taasisi za watu binafsi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai