Ushirikiano Katika Jamii Utasaidia Kupunuza Unyanyasaji wa Watoto
Imetumwa: April 22nd, 2021
HaiUshirikiano kati ya wazazi na walezi ukiimarishwa katika haki na ulinzi wa mtoto itasaidia kupunguza ukatili unaotendeka dhidi ya watoto kwenye jamii.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Isawerwa Kata ya Romu wilayani Hai Afisa Maendeleo ya Jamii Esther Msoka amesema ushirikiano wa ulinzi wa mtoto ukiimarishwa na wananchi kuelewa madhara ya ukatili kwa watoto itasaidia kuhakikisha ulinzi wa mtoto unakuwepo wakati wote.
Amefafanua kuwa Serikali kwa kuona umuhimu wa malezi chanya kwa mtoto imeweka jitihada mbalimbali za kuhakikisha ulinzi wa mtoto ikiwemo sheria ya mtoto na mkataba wa kimataifa wa kumlinda mtoto.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Hai Helga Simon ameeleza kuwa wazazi na walezi wana wajibu mkubwa wa kuwalea watoto katika malezi chanya yatakayopelekea kutokomeza ukatili kwenye jamii.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa kijiji cha Isawerwa Bw. Obedi Munisi na Bi. Upendo Kimaro wameeleza kuwa ukatili uliokuwa ukitendeka kwenye baadhi ya familia kijijini hapo umepungua kwa sasa kutokana Elimu ya mara kwa mara ambayo imekuwa ikitolewa na serikali.
Kulingana na mpangokazi wa kuzuia ukatili dhidi ya mtoto unaeleza kuwa asilimia 72 ya ukatili wanaofanyiwa watoto unatoka kwa watu wa karibu na familia.