USHIRIKIANO mzuri uliopo kati ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro na watumishi katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani umefanikisha kutolewa kwa wakati mikopo kwa vikundi vya wanawake vijana watu wenye ulemavu.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Amiri Mkalipa ameyasema hayo wakati akikabidhi hundi ya shilingi milioni mia mbili na nne kwa ajili ya kukopesha vikundi 27 vilivyokidhi vigezo vya kukopeshwa na Halmashauri kutokana na makusanyo ya mapato ya ndani.
“Niwapongezee sana madiwani wa halmashauri kwa ushirikiano wenu, leo tunaona matunda yake, mmefanya kazi kubwa sana ya kusimamia mapato hali ambayo kwa sasa tunaona kila robo ya mwaka vikundi vinanufaika na mikopo”
“Kazi mnayoifanya kila siku inaoneka na mnatekeleza ilani kwa vitendo kwa ufuatiliaji mnaofanya kila mara umesaidia kuimarisha na kuongeza mapato ya ndani na leo tumeoa vikundi 27 vinapatiwa mkopo kwa ajili ya kufanya shughuli za kujikwamua kiuchumi”alisisitiza mkuu wa Wilaya
Amesema mikopo hiyo isiyokuwa na riba inayotolewa na Serikali ya awamu ya sita lengo lake ni kuwainua wananchi kiuchumi na kuondokana na hali ya utegemezi na badala yake kila mmoja aweze kuwa na mafanikio yake binafsi ambayo yataweza kusaidia kuondokana na umasikini.
Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya amewataka wanufaika wa mkopo huo, kuhakikisha fedha walizozipata zinafanya kazi iliyokusudiwa na kuacha tabia za kubadilisha matumizi jambo ambalo linaweza kusababisha kupoteza fedha hizo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kuhakikisha wanarejesha fedha hizo kwa wakati ili kuwezesha wananchi wengine wa wilaya hiyo kukopeshwa fedha hizo zisizokuwa na riba kwa lengo la kwenda kufanya shughuli za kujikwamua kiuchumi.
“Nachukua fursa hii kuwapongeza kwa kupata mikopo ambayo itakwenda kuwanufaisha ninyi pamoja na familia zenu, Mwenyezi Mungu awawezeshe mkatimize malengo na kurejesha kwa wakati ili wengine wakope”
Afisa maendeleo ya jamii wilaya hiyo Robert Mwanga amefafanua kuwa tangu mwezi Julai 2022 hadi Machi 2023 Halmashauri imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 346 kwa vikundi 31 ambapo vikundi 17 ni vya wanawake, vijana ni vikundi 12 na vikundi vya watu wenye ulemavu 02 huku watu binafsi 10 wenye ulemavu.
“Mheshimiwa mkuu wa Wilaya Halmashauri imeweza kuchangia kiasi chote kilichopaswa kuchangiwa kama inavyoelekezwa katika sheria ya fedha ya Serikali za mitaa ya mwaka 1982 na marekebisho yake ya mwaka 2012”
Amefafanua kuwa tangu mwezi Julai 2022 hadi Machi 2023 Halmashauri imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi 346,125,172 kwa vikundi 31 ambapo vikundi 17 ni vya wanawake, vijana ni vikundi 12 na vikundi vya watu wenye ulemavu 02 huku watu binafsi 10 wenye ulemavu .
Alieleza kuwa kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi 132,481,172 zinatokana na asilimia kumi ya mapato ya ndani na kiasi cha shilingi 213,644,650 zinatokana na marejesho ya vikundi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai