Imeelezwa kuwa faini mbalimbali ikiwemo ya shilingi milioni moja au kifungo cha miezi 12 jela, ama adhabu zote kwa pamoja, zinawasubiri wakazi wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, wanaoharibu mazingira kwa kulisha mifugo kwenye miti iliyooteshwa au kukata miti bila ya kuwa na kibali cha serikali.
Akizungumza katika kampeni ya upandaji miti kwenye Kituo cha Afya Longoi, kilichopo Kata ya Weruweru, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Edmund Rutaraka, alisema uamuzi wa kuwabana wanaoharibu mazingira unalenga kuongeza msukumo wa kukabiliana na tatizo hilo.
Mkurugenzi wa Shirika la Voice of Empowered Women Foundation, ambalo linaendesha kampeni hiyo ya utunzaji wa mazingira Asifiwe Mallya, alisema wamelenga kuboresha mazingira kwa kupanda miti 500 katika Kituo hicho cha Afya Longoi, ambacho kinatishiwa na ukame.
Ofisa Mazingira wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Kanda ya Kaskazini, Albert Loti, akizungumza na wananchi wa Longoi, alisema kazi kubwa inayofanywa hivi sasa ni kutoa elimu zaidi kuhusiana na upandaji miti, matumizi ya mifuko ya plastiki, uchafuzi wa mazingira kwa njia ya sauti na namna nyingine mbalimbali.
Ofisa Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Mbayan Mollel, alisema kwa mwaka 2020/2021, takribani miti 899,876 ilipandwa hadi kufikia Juni 30 mwaka jana katika maeneo ya milimani na tambarare, sawa na asilimia 60.
Kwa mujibu wa Mollel, kwa mwaka 2021/2022 ambao bado unaendelea, mpaka kufikia sasa Wilaya hiyo imepanda miti 595,859, sawa na asilimia 39.7 ya malengo.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai