Serikali katika Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imewaelekeza wakuu wa shule zilizopokea wanafunzi wa Kidato cha Sita kusimamia taaluma na kuimarisha juhudi za kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo wakati wa kupokea msaada wa vifaa vya kunawia mikono; Katibu Tawala wilaya ya Hai Upendo Wella amesema Serikali imeamua kuwarudisha shuleni wanafunzi wa vyuo vikuu na kidato cha sita ili wajiandae na mtihani wao wa kumaliza elimu ya sekondari.
Amesema Serikali inamthamini kila mwanafunzi na mwalimu hivyo nao wasibweteke bali waendelee kuchukua tahadhari za kujikinga na maambukizi kama inavyoelekezwa na wataalamu wa afya.
“Tunaamini kuwa tukiendelea kuchukua tahadhari za kunawa mikono na kukaa kwenye umbali unaoelekezwa itafika siku ugonjwa huu utapotea” Amesisitiza.
“Ipo haja ya kuendelea kufuata taratibu hizo ili kutokomeza magonjwa mengine yanayotokana na uchafu. Wataalamu wa afya wanashuhudia kuwa idadi ya wagonjwa wa magonjwa mengine wanaofika hospitali kutibiwa imepungua sana” ameongeza Wella.
Akikabidhi msaada huo Mchungaji Mmisionari Julias Nkya wa makanisa ya Free Pentecostal yanayofanya kazi nchini Tanzania nan je ya nchi amesema wameona umuhimu wa kushirikiana na Serikali katika mapambano ya ugonjwa wa Corona.
Amesema kuwa kanisa lao linashiriki kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kupambana na ugonjwa huu hususani katika kujikinga na maambukizi pamoja na kusaidia vifaa kama ndoo na sabuni kwa ajili ya kunawia mikono ambayo mpaka sasa ndio njia kuu ya kujikinga na maambukizi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amewashukuru wahisani hao kwa mdaasa walioleta lakini pia kwa namna wanavyotekeleza wajibu wa kuielimisha jamii katika kujikinga na ugonjwa wa Corona.
Aidha Mkurugenzi Sintoo ameelekeza baadhi ya vifaa hivyo kupelekwa kwenye shule za sekondari zenye wanafunzi wa Kidato cha Sita ili kusaidia wanafunzi kujikinga na ugonjwa huo.
Kanisa la Free Pentecostal Church of Tanzania kupitia mradi wa “Tuna Ndoto” wamekabidhi vifaa vya kunawia mikono ikiwemo ndoo na sabuni za kunawia mikono 100 zenye thamani ya shilingi millioni 2.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai