Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imetoa wiki moja kwa wajasiriamali wadogo wanaostahili kuwa na vitambulisho vinavyotolewa na Serikali kufanya hivyo ili kuwapa uhuru wa kufanya biashara zao.
Akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Sadala, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Yohana Sintoo amewataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa na kujipatia vitambulisho hivyo.
“Mimi kama Mkurugenzi wa Halmashauri na Msimamizi wa soko hili; nawapa siku saba kwa wafanyabiashara wadogo kuchukua vitambulisho. Baada ya muda huo hakuna mfanyabiashara atakayeruhusiwa kufanya biashara ya aina yoyote kwenye mipaka ya halmashauri yetu” Amesisitiza Sintoo.
Mkurugenzi Sintoo akiongozana na Wakuu wa Idara na Vitengo, Watendaji wa Kata na Vijiji wa halmashauri yake ametembelea maeneo ya masoko ikiwemo soko la Sadala kwa ajili ya kuwaelimisha na kuwahamasisha wafanyabiashara umuhimu wa kuwa na kitambulisho cha mjasiriamali mdogo.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Magufuli ametoa vitambulisho hivi ili kuwaondolea wafanyabiashara wadogo adha ya kulipa ushuru kila wanapofanya biashara zao” ameongeza Sintoo.
Kwa upande mwingine Afisa Biashara wilaya ya Hai Ernest Mhapa amewataka wafanyabiashara kutambua kuwa vitambulisho walivyochukua mwaka jana vimekwisha muda wake hivyo wanatakiwa kuchukua vitambulisho vipya vya mwaka 2020.
Mhapa amesema kuwa utaratibu wa kupata vitambulisho hivi unasaidia wafanyabiashara wadogo kuingia kwenye kanzidata ya Serikali huku kila mfanyabiashara akitambulika kwa jina, picha na namba ya kitambulisho anachomiliki.
Zoezi la kugawa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo linaendelea nchi nzima kama lilivyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuwapunguzia wafanyabiashara wadogo idadi ya kodi wanazotakiwa kulipa. Vitambulisho hivi vinapatikana kwa Sh. 20,000 na kinatumika kwa muda wa mwaka mmoja.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai