Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya amewaagiza wakandarasi wanaofanya matengenezo kwenye barabara ya Bwani –Kyeeri kukamilisha kazi hiyo kwa wakati kulingana na mkataba waliopewa ambao unaonyesha kuwa kazi hiyo inapaswa kukamilika tarehe kumi na tano mwezi Machi mwaka 2019.
Sabaya ametoa agizo hilo wakati akizindua matengenezo ya barabara ya Bwani-Kyeeri inayoziunganisha kata za Machame Magharibi na Machame Uroki, tukio lililofanyika katika Kijiji cha Bwani kata ya Machame Uroki.
“Bila shaka umeshanisikia kiasi, ikipita maana yake ni mimi na wewe sawa sawa, ila ikikamilika ndani ya muda tutakupongeza” amesema Sabaya.
“Kampuni moja inatuma zaidi ya shilingi milioni 145 na nyingnie inatumia zaidi ya shilingi 4000 hizi ni fedha kubwa na ni fedha za wananchi walipa kodi, Rais ameruhusu fedha hizi zitumike kwa kuwa kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi kuna maelekezo ya kujenga barabara kwa hiyo muhakikishe mnazitumia vizuri” alisisitiza Sabaya.
Kwa upande mwingine Sabaya amewataka wananchi wa kata hizo kutoa ushirikiaono kwa wakandarasi ili waweze kufanya kazi kwa urahisi huku akiwaagiza wakandarasi kufanya kazi hiyo kwa uangalifu bila ya kuwasumbua wananchi wakizingatia uaminifu.
Naye Menejea wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Hai Mhandisi Charles Marwa amesema kwa mwaka 2018/2019 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni moja milioni mia tatu na mbili kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Wilaya hiyo.
Ameongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha km 2.5 zitatengenezwa kwa gharama ya shilingi milioni 44 kwenye barabara ya Bwani- Kyeeri yenye jumla ya kilomita 9.7 yatakayozingatia matengenezo ya sehemu korofi na changarawe.
Amesema matengenezo hayo yatawasaidia wananchi kutatua changamoto za usafiri zilizokuwa zinawakabili hasa Bwani, Kyeeri, Uraa na vijiji vya jirani vya Uswaa kwa kuwa vijiji hivyo vimekuwa na changamoto ya muda mrefu ya barabara kutopitika hasa wakati wa mvua na kusababisha baadhi ya huduma muhimu za jamii kutowafikia wananchi kwa wakati.
Nao madiwani wa kata mbili zinazopitiwa na barabara hiyo; Martini Munisi wa Machame Magharibi na Robson Kimaro wa Machame Uroki kwa pamoja wamemshukuru na kumpongeza Mkuu wa Wilaya pamoja na Rais John Pombe Magufuli kwa hatua hiyo iliyolenga kuwasaidia wananchi.
“Wananchi wangu wa Kyeeri wameniambia tangu tupate uhuru kwa mara ya kwanza yamefanyika matengenezo ya kihistoria, matengenezo mazuri na yenye hadhi ambayo hayajawahi kufanyika” alisisitiza Munisi huku akiwataka wananchi hao kutunza barabara kwa kuheshimu sheria za barabarani.
Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 katika awamu ya kwanza TARURA wilaya ya Hai inatarajia kutekeleza mikataba mitatu ya matengenezo ya barabara yenye thamani ya shilingi 605,109,971 ambayo itatekelezwa na wakandarasi wawili ambao ni NURE building and civil contractors na ATHU building and civil works Jv advanced CO.LTD.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai