Serikali imeanza kuwaandaa wananchi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kuendelea kupata tija kwenye shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi.
Mkuu wa Kitengo cha Mazingira cha Wizara ya Kilimo Shakwanande Natai kinachoshughulikia uratibu wa hifadhi ya mazingira na uhimili wa mabadiliko ya tabiachi amesema mkakati wa serikali unalenga kuboresha uzalishaji
“Mabadiliko ya tabianchi yamesababisha ukame usioelezeka ambao unasababisha mazao hayafiki mwisho kuleta mavuno mazuri na kusababisha uzalishaji wa chakula kupungua ” Amesema Natai.
Amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zinaongezeka na kusambaa kwenye maeneo mengi kiasi cha kuhatarisha upatikanaji wa chakula kutokana na umuhimu wa sekta zinazokubwa.
Natai ameendelea kusema kuwa sekta ya kilimo inategemewa kama nguzo muhimu ya uchumi nchini na inajumuisha uzalishaji wa mazao, mifugo na uvuvi na inachangia kutoa ajira kwa zaidi ya asilimia 65 ya watanzania.
Ameongeza kuwa sekta hiyo inachangia asilimia 95 ya mahitaji ya chakula kwa Taifa pamoja na kwamba ina mchango wa nusu ya pato la Taifa .
Natai amebainisha kuwa serikali kwa kupitia Wizara ya Kilimo imeandaa mwongozo wa kilimo unaohimili mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2017 unaoainisha mbinu na teknolojia za kuwaongoza watunga sera na watoa maamuzi, maafisa ugani, wakulima, wafugaji na wavuvi ili kukabiliana na mabadiliko hayo.
“Wizara imetengeneza kijarida chenye taarifa za mbinu na teknolojia zinazohusiana na kilimo, mifugo na uvuvi kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kuelewa na kutekeleza kazi zao kwa kutumia mwongozo”
“Tumefika Wilaya ya Hai kwa lengo la kusambaza mwongozo huu pamoja na kuwaelimisha wataalamu wa halmashauri wanaoshughulika na kilimo, mifugo na uvuvi ili waweze kuwasaidia wakulima kupambana na mabadiliko” Ameongeza Natai.
Naye Afisa Kilimo Wilaya ya Hai David Lekei amesema wamefarijika kupata mwongozo huo na kwamba wapo tayari kushirikiana na wakulima ili kuboresha upatikanaji wa chakula.
Kwa upande mwingine Afisa Habari wa Halmashauri Riziki Lesuya amesema atashirikiana na idara husika kuwafikishia wananchi taarifa za namna ya kukabiliana na athari za tabianchi kwa kutumia vyombo vya habari na aina mbalimbali za mawasiliano ili kila mwananchi apate tarifa sahihi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai