Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Stephen Kagaigai amewataka Wakuu wa Wilaya walioapishwa kuhudumu katika wa mkoa huo kutumia muda wao wote kuwahudumia wananchi kwenye wilaya zao.
Akihutubia hadhara iliyoshuhudia kiapo cha wakuu hao wa wilaya; Kagaigai amesema amewahi kuona tangazo kwenye ofisi za wakuu wa wilaya likielekeza siku za wananchi kukutana na mkuu wa wilaya ofisini. Wengi ikionesha kuwa wananchi wanapata nafasi ya siku moja kukutana na Mkuu wa Wilaya.
Kagaigai amesema ni wajibu kwa wakuu wa wilaya kuwasikiliza wananchi muda wowote kadri patakapotokea uhitaji.
Aidha, Kagaigai amewakumbusha wakuu wa wilaya kutumia kwa umakini na usahihi utaratibu wa kuwaweka kizuizini wananchi wanaohatarisha usalama ndani ya wilaya zao.
“Nadhani wengine kwa kutokujua wamekuwa wakikurupuka na kuwaweka watu kizuizini” Amefafanua Kagaigai.
Amesema kuwa hatua ya kuweka mahabusu watumishi au wananchi ni jambo linalohitaji kufanywa kwa umakini na ikiwezekana mkuu wa wilaya anayetaka kutekeleza hilo anaweza kumshirikisha ili kwa pamoja washauriane.
Pamoja na wito huo Kagaigai amewataka viongozi na wananchi wote wa Mkoa wa Kilimanjaro kusimamia na kuzingatia tahadhari za ugonjwa wa corona kama inavyoelekezwa na Wizara ya Afya.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro amewaapisha Wakuu wa Wilaya wapya 2 na kuwapokea wakuu wa wilaya 3 waliohamia kutoka mikoa mingine na mkuu mmoja wa wilaya aliyebadiishiwa kituo ndani ya mkoa huo.
Walioapishwa ni Abdallah Mwaipaya (Mwanga), Kanali Hamis Maiga (Rombo), waliohamia kutoka mikoa mingine ni Juma Irando (Hai), Edward Mpogolo (Same) na Said Mtanda (Moshi) huku aliyebadilishiwa kituo ndani ya mkoa akiwa Thomas Apson aliyekuwa Wilaya ya Mwanga na kuhamishiwa Wilaya ya Siha.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai