Wito umetolewa kwa walimu kuwa chachu ya tabia njema na mwenendo bora kwa kuishi maisha ya mfano kwa wanafunzi wao na jamii kwa ujumla katika kutekeleza majukumu ya kazi pamoja na kuwa wazalendo kwa kutanguliza mbele maslahi mapana ya taifa.
Akizungumza katika hafla ya kuwatunuku vyeti walimu wa shule mbalimbali za msingi na sekondari iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Hai Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Edward Ntakiliho amesema halmashauri itaendelea kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha kuwa shule zote za msingi na sekondari zinapeleka walimu kwenye mafunzo hayo na kupata wakufunzi wa skauti.
“Kuanzia sasa tunategemea walimu na wanafunzi wakiongozwa na mwalimu wa skauti watakuwa wazalendo kwa nchi, watakuwa watetezi wa mambo mema kwa jamii na kukemea vitendo viovu” ameongeza Ntakiliho.
Kwa upande wake Kamishna wa Skauti mkoa wa Kilimanjaro Bright Matola amesema kuwa lengo la mafunzo hayo kwa walimu ni kuwafanya wakawe mabalozi wazuri kwa wanafunzi wao katika vituo vyao vya kazi kwani kufanya hivo ni imani kuwa wanafunzi watakuwa wakakamavu kutokana na mafunzo watakayopata kutoka kwa walimu hao.
Aidha Matola amebainisha kuwa jumla ya walimu 146 wamehitimu mafunzo hayo na kutunukiwa vyeti vyao hii leo ikiwa ni kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari za serikali pamoja na shule binafsi ambao wameitikia wito huo.
Akizungumzia ushiriki wa Wilaya ya Hai; kamishna wa skauti wilaya hiyo Upendo Fredrick amesema kuwa mafunzo hayo yatajenga walimu bora ndani ya wilaya huku akitoa wito kwa shule ambazo hazijapeleka walimu katika mafunzo hayo kufanya hivyo kwenye mafunzo yatakayoendelea kutolewa kwenye wilaya nyingine ikiwemo wilaya ya Siha itakayoanza mafunzo hayo mwishoni mwa wiki hii.