Wanafunzi watatu wanaosoma masomo ya Dini Katika Chuo kinachotoa mafunzo ya Quran na hadithi za Mtume cha Othuman Binhassan kilicho chini ya Msikiti wa Othman Bomang’ombe Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wakituhumiwa kuchoma moto bwalo la chakula linalotumiwa na wanafuzi wa chuo hicho.
Tukio la kuchomwa moto bwalo hilo limetokea Jumapili ya tarehe 11 Octoba 2020 wakati waumini wa msikiti huo wakiendelea na Swala ya adhuhuri ambapo kufuatia tukio hilo mkuu wa wilaya ya Hai ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya Lengai Ole Sabaya amefika msikitini hapo kukagua athari na kupata taarifa ya tukio hilo.
Sabaya amesema kuwa tayari Jeshi la Polisi wilayani humo linawashikilia wanafunzi watatu ambao wamekiri kuhusika na tukio hilo huku akilipongeza jeshi la polisi kwa jitihada walizofanya kwa muda mfupi za kufanikisha kuwakamata na kulitaka jeshi hilo kuendelea na uchunguzi ili kubaini sababu za tukio hilo.
“OCD mimi nakupongeza sana wewe na vijana wako kwa kazi mliyoifanya ya kuhakikisha kwamba angalau tumetatua kitendawili cha nani amechoma, hili ni tukio letu la kwanza kwenye wilaya ya Hai na tulikubaliana kwamba kwenye wilaya hii matukio ya namna hiyo hayatatokea”. Amesema Sabaya.
“Hapa tumepata watu watatu ambao wamethibitika wamechoma moto jengo hilo, kwa hiyo muendelee kuwahoji vizuri wawaambie kama kuna wengine na waseme wanafanya project ya nani na walitaka kuwauwa wangapi ili tufikishe hitimisho hii ajenda mpya yakuchoma maeneo na taasisi mbalimbali”. Ameongeza Sabaya.
Aidha Sabaya ameuomba uongozi wa msikiti na chuo hicho kuhakikisha kuwa unaendeleza uhusiano mzuri baina yao na serikali kwani kwa kupitia ushirikiano wa katibu ni rahisi kubadilishana taarifa na kuweza kuzuia vitendo vya uhalifu kabla havijatokea.
Awali akisimulia tukio hilo Msimamizi Mkuu wa chuo hicho na imamu wa msikiti huo Abdala Juma amesema kuwa kabla ya tukio la moto kulitokea upotevu wa simu za wanafuzi 68 ambazo ziliibiwa na wanafuzi hao watatu na kwenda kuzificha kwenye dari la msikiti ambapo amesema kuwa walipowahoji wanafunzi hao walisema kuwa waliamua kuchoma jengo hilo moto ili chuo kifungiwe na wao wapate fursa yakutoroka na simu hizo.
“Tuna utaratibu wanafunzi wote wakifika simu zao tunazichukua na kuziweka kwenye chumba cha kiongozi, watuhumiwa hao walivizia tukiwa msikitini wakaiba zile simu zote wakazificha na baada ya hapo tukafanya uchunguzi wakahisi tutawakamata.”
“Baada ya tukio tuliwahoji wakasema waliamua kuwasha moto ili chuo kifungwe na kikishafungwa wapate fursa ya kuchukua zile simu waondoke nazo kutoka mahali walipozificha juu ya dari ndani ya msikiti”. Amesema Imamu Abdala Juma.
Kuhusu madhara amesema kuwa moto huo umeteketeza magodoro 8, mabegi sita na nguo chache za wanafuzi huku vitu vingine vikiokolewa.
Hivi karibuni kumekuwa na mfululizo wa matukio ya kuungua kwa moto mabweni katika shule mbalimbali hapa nchini ambapo mpaka hivi sasa jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi katika matukio hayo ili kubaini chanzo chake.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai