Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Bomboko, amesema wananchi wa wilaya hiyo wako tayari kwa mchakato wa uchaguzi, wakichochewa na mafanikio makubwa ya maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Zainab Katimba, aliyefanya ziara wilayani humo, Bomboko amesema zaidi ya shilingi bilioni 56 zimetumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika wilaya ya Hai.
"Kwa kipindi cha miaka minne ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, zaidi ya shilingi bilioni 56 zimetumika kwa ajili ya maendeleo hapa Hai. Mwambieni Mheshimiwa Rais akae kwa amani, wilaya ya Hai ina usalama. Kazi yetu sisi viongozi ni kwenda kuwaeleza wananchi mafanikio haya makubwa ambayo wameyaona kwa macho yao," amesema Bomboko.
Aidha, DC Bomboko amesema tayari zoezi la kujiandikisha limekamilika, na wananchi wengi wamejitokeza kwa wingi, jambo linaloashiria utayari wao kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi ujao.
"Wananchi wa Hai hawazungumzii reform nyingine zaidi ya maendeleo. Na maendeleo tayari wanayo. Wanatambua juhudi za serikali yao, na wameahidi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi," ameongeza.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Hai, Saasisha Mafuwe, amesema wananchi wa wilaya hiyo wamefunguka macho na kutambua kuwa maendeleo ndiyo ajenda kuu.
"Hizi habari za reform wananchi wa Hai hawazitaki. Wanatambua kuwa Mheshimiwa Rais ametuletea fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya kijamii iliyoigusa jamii moja kwa moja. Ametufanyia mambo makubwa sana ndani ya wilaya yetu," amesema Mafuwe.
Naibu Waziri Zainab Katimba alipongeza utekelezaji wa miradi katika wilaya hiyo na kusisitiza umuhimu wa kushirikiana na wananchi ili kuhakikisha maendeleo yanaendelea kuletwa kwa tija.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai