Wananchi katika kata za Machame Uroki na Kia Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la kupiga kura kuchagua viongozi wanaowataka kwenye uchaguzi mdogo utakaofanyika septemba 16 kwenye kata hizo.
Akizungumza na Redio Boma FM mapema leo tarehe 13/09/2018, Afisa uchaguzi kutoka tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Magreth Chambiri amewakumbusha wananchi kuwa ni marufuku kwenda kwenye kituo cha kupigia kura wakiwa wamevaa vazi lenye nembo ya chama.
Chambiri amesema hayo wakati wa kutoa elimu kwa wapiga kura kuelekea uchaguzi huo wa madiwani utakaofanyika katika kata mbili zilizopo katika jimbo la Hai ambapo amewahamasisha wananchi kushiriki zoezi la uchaguzi kwani ni haki yao.
“Niwahimize wananchi wa maeneo yenye uchaguzi kufika kwenye vituo vya kupigia kura wakiwa na kadi ya kupigia kura au utambulisho mbadala na kuchagua viongozi wanaowataka” Amesisitiza Chambiri.
Sanjari na hayo ameongeza kuwa wananchi wanao wajibu wa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa katika chaguzi hizo kwani utulivu na kufuata sheria kutapelekea wao kuwa salama na kupata kiongozi bora wa kuwawakilisha na kutatua kero zinazowakabili katika maeneo yao.
Akikagua maandalizi ya chaguzi hizo Kamishna wa Uchaguzi Taifa Omar Mapuri amewataka wasimamizi wa uchaguzi huo kufuata sheria na kanuni kama walivyoelekezwa kwenye semina ya kuwaandaa kusimamia uchaguzi huku akiwataka kila mmoja kuwajibika kulingana na majukumu yake.
Kwa upande wake Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Hai Yohana Sintoo amewataka wasimamizi wa uchaguzi kuwa makini wakati wa kutekeleza majukumu yao siku ya uchaguzi.
“Dhamana mliyonayo ni kubwa sana kwani zoezi hili ni muhimu linalohitaji umakini mkubwa; nawaombeni sana mzingatie sheria za uchaguzi kama mlivyofundishwa kwenye semina” Amesema Sintoo.
“Msimamizi au msimamizi msaidizi akitumiaa vibaya madaraka yake na kusababisha matokeo ya uchaguzi kubatilishwa atakabiliwa na faini au kifungo au vyote viwili kama inavyoelezwa kwenye sheria ya uchaguzi, hivyo ndugu zangu nawaomba muwe makini katika kutekeleza majukumu yenu ” Ameongeza Sintoo.
Uchaguzi Mdogo wa marudio unafanyika kwenye kata za Machame Uroki na Kata ya Kia baada ya waliokuwa madiwani katika kata hizo hivi karibuni kujiuzulu nafasi zao za Udiwani ambazo walikuwa wakizitumikia kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na badae kuhamia katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai