Msimamizi wa uchaguzi wa Halmashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Juma Masatu amewahimiza wananchi kujitokeza katika vituo vya uandikishaji wa orodha ya daftari la wapiga kura ambapo zoezi hilo limeanza rasmi leo Octoba 8.
Masatu ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na Redio Boma Hai FM katika kipindi cha TukoPamoja na kubainisha kuwa zoezi hilo la uandikishaji linafanyika katika ofisi za vitongoji ambapo waandikishaji wapatao 294 wameshapelekwa katika vituo vyote kwa lengo la kusimamia zoezi hilo.
Aidha Masatu amezitaja sifa za mtu anayepaswa kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura, kuwa ni lazima awe raia wa Tanzania pia awe na umri usiopungua miaka 18 na kuendelea.
Sifa nyingine ambazo amezitaja Masatu ni pamoja na mhusika kutoka katika kijiji/kitongoji anachoishi, pia kuwa na akili timamu
Amebainisha kuwepo kwa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu ,wazee, pamoja na akina mama wajawazito na wenye watoto wadogo huku akiwataka wanafunzi wenye sifa za kujiandikisha kwenda katika ofisi ya kitongoji kilichopo karibu na shule kwa ajili ya kujiandikisha.
Uandikishaji wa wananchi katika orodha ya wapiga kura unafanyika kuanzia leo octoba 8 na kukamilika octoba 14 2019, ambapo uchaguzi huo utafanyika Novemba 24 mwaka huu utakaokwenda sambamba na kuwachagua wenyeviti wa vijiji na vitongoji pamoja na kuwachagua wajumbe wa halmashauri za vijiji.
Kwa mujibu wa sheria ya serikali za mitaa mamlaka za wilaya sura ya 287 inaeleza kuwa mtu hatakuwa na haki ya kupiga kura endapo hana moja wapo ya sifa zilizoainishwa katika kanuni ya 12 au amejiandikisha kupiga kura katika kituo zaidi ya kimoja.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai