Wananchi Wamehimizwa Kuanzisha Kusajili Vikundi Kupata Mikopo ya Halmashauri
Imetumwa: April 25th, 2021
Diwani wa kata ya Masama kati Kandata Kimaro amewataka wanawakena vijana katika kitongoji cha Marukeni kijiji cha Ng'uni kuunda vikundi kwa wingi na kuvisajili ili kukidhi vigezo vya kupata mikopo isiyokuwa na riba katika halmashauri ya wilaya ya Hai.
Aidha diwani Kandata ametoa hamasa kwa walemavu ambao ni wajasiriamali waliopo katika kata hiyo kujitokeza kupata fursa za mikopo kwa kuwa mlemavu hupatiwa mkopo hata akiwa peke yake bila kujiunga kwenye kikundi.
Ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa vikundi viwili vya wanawake wajasiriamali katika kata hiyo ikiwemo kikundi cha Mapinduzi chenye wanachama 30 pamoja na kikundi cha Furahini chenye wanachama 22.
"Niwaombe wakina mama muwahamasishe vijana kuunda vikundi kwa wingi wapate mikopo" amesema diwani Kandata na kuongeza kuwa
"Kata yangu ya Masama kati toka nimekuwa diwani zilitolewa milioni 159 lakini kata yangu imepata kikundi kimoja tena milioni 7 tu naulizwa diwani huna vijana, huna walemavu" amesema Kandata.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi cha Mapinduzi Bi. Akwiyande Ndosi ameeleza kufurahishwa na mwitikio wa diwani wa kata hiyo kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa vikundi hivyo kwa lengo la kuwainua wanawake wa eneo hilo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kikundi cha Furahini Mama Anna Urassa amesema kuwa wameamua kutumia nguvu ya pamoja kuungana kwa lengo la kupata mikopo kwa ajili ya kujiinua kiuchumi.
Vikundi hivyo viwili vya Mapinduzi na Furahini vilianzisha February 2021 vikiwa na lengo la kuunganisha nguvu ya pamoja kwa wanawake na kupata mikopo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.