Wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai wametakiwa kujenga mazoea ya kupanda miti kila inapofika kipindi cha mvua ili kuimarisha mazingira yanayowazunguka.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Hai Upendo Wella wakati akizindua wiki ya upandaji miti katika wilaya hiyo.
Wella amesema ili kuwa na mazingira rafiki kwa ajili ya binadamu na viumbe vingine ipo haja ya wananchi kupanda miti kwa wingi kwani uwepo wa mitiya kutosha unasaidia kuboresha maisha ya viumbe hai.
Ametumia uzinduzi huo kuwakumbusha wananchi wa maeneo ya Bomang’ombe hali ilivyokuwa miaka minne iliyopita na kukiri kuwa mazingira yameimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na juhudi zinazochukuliwa za kupanda miti na kutunza mazingira.
Aidha Wella amewahamasisha wananchi kuanza kujihusisha na kilimo cha zao la korosho ambalo limetambulishwa katika Wilaya ya Hai baada ya utafiti kubaini zao hilo kustawi maeneo ya ukanda wa chini wa wilaya hiyo.
“Niwahimize kuanza kilimo cha korosho kwa sababu ni moja ya mazao ya kimkakati yanayopigiwa chapuo na Serikali lakini pia ni chanzo kikubwa na cha uhakika cha kipato kwa mtu mmojammoja na hatimaye kwa Taifa zima” Amesema Wella.
Kwa upande wake Afisa Maliasili Wilaya ya Hai Mbayani Mollel amesema kuwa jumla ya miti 3000 imepandwa siku ya uzinduzi katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Kituo cha Polisi Wilaya pamoja na Hospitali ya wilaya ya Hai na kwamba zoezi la upandaji litaendelea kwenye taasisi za Serikali ikiwemo vituo vya huduma za afya, shule na ofisi za Umma.
Mollel amesema kwamba Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepanga kuotesha miti milioni moja na laki tano kila mwaka ili kuimarisha mazingira, kutokomeza hali ya jangwa na kuifanya dunia makazi salama kwa wanadamu na viumbe wengine.
Naye Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la VOEWOFO Asifiwe James ambaye shirika lake ni mdau wa masuala ya kijamii amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika masuala yote yanayohusu ustawi wa wananchi ikiwemo kuotesha na kutunza miti kwani kwa kufanya hivyo wanachangia kuboresha maisha ya wananchi.
Kila mwaka maadhimisho ya wiki ya upandaji miti hufanyika kwa kuotesha miti ya matunda na kivuli kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo taasisi za umma na kuendelea kuwahamasisha wananchi kupanda na kutunza miti kwenye maeneo ya makazi na biashara.