Katibu tawala wilaya ya Hai Upendo Wella amewataka watumishi wa umma na wananchi wilayani Hai kuendelea kujitokeza kupata chanjo ya Uviko-19 kwa lengo la kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo na kuwahakikishia wananchi kuwa chanjo salama.
Wella ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Siku mpya kinachorushwa na Redio Boma Hai fm na kuwataka watumishi wa umma wale ambao hawajachanjwa kuwa mstari wa mbele kwa kuonyesha mfano kwa jamii katika zoezi la uchanjaji.
“wale ambao bado hawajafanya maamuzi waendelee kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupata chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa Uvico-19 na pia waendelee kujitokeza kuchanja pale wanapowaona wataalamu wa Afya wamekuja kwenye maeneo yao lakini pia katika vituo ambavyo vimepangwa kwa ajili ya wao kwenda kupata chanjo hiyo”
Aidha wilaya ya Hai imeongoza kwenye zoezi la utoaji wa chanjo katika ngazi ya mkoa baada ya kupokea chanjo ya Jansen kutoka kampuni ya Johson & Johnson awamu ya kwanza na ya pili ambapo jumla ya chanjo 12, 560 zilipokelewa na zilizotolewa kwa wananchi ni 11, 993 sawa na asilimia 95.5 ya chanjo hizo.
Katika hatua nyingine katibu tawala Upendo Wela, amewapongeza watumishi wa Afya katika Hospitali ya wilaya ya Hai wakiongozwa na mganga mkuu Dkt. Irene Haule kwa juhudi walizozionesha kuwafikia wananchi na kuwapatia huduma hiyo.
Naye mganga mkuu wa wilaya ya Hai Dkt. Irene Haule akielezea kuhusu zoezi la chanjo amesema kuwa tayari wilaya hiyo imeshapokea chanjo aina ya Sinopharm zipatazo 4824 na kusambazwa katika vituo 46 vya kutolea huduma za Afya na kuwataka wananchi kujitokeza kuchanja kwani kuchanja ni faida na kutochanja ni hasara.
“Watu waelewe kuwa ni muhimu katika maeneo yao kila mmoja akawa amepata chanjo kwa wale wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea wapate chanjo ili kuweza kupata kinga, kuna faida nyingi sana katika kuchanja lakini kuna hasara kubwa sana kwa kutokuchanja”
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai