Wananchi kutoka kata ya Bomang’ombe wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, wameishukuru serikali kwa kuratibu vyema zoezi la kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ambalo linaendelea katika kituo cha Geza Ulole.
Wakizungumza na Redio Boma Hai FM, baadhi ya wananchi wamesema kuwa zoezi hilo limeendeshwa kwa haraka, kwa usalama, na bila usumbufu mkubwa kama ilivyokuwa ikihofiwa na baadhi ya watu.
"Kwa kweli serikali imejitahidi. Nimekuja hapa Geza Ulole saa tatu asubuhi, lakini mpaka saa nne tayari nimeshajiandikisha. Hakuna msongamano, hakuna matusi, kila mtu anatendewa sawa," alisema Manka Shirima, mama wa watoto watatu.
Lembris Mollel alisema licha ya upotoshaji unaoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uchaguzi, yeye na vijana wenzake wameamua kujiandikisha ili kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura. "Hii ni haki yetu. Tusipojiandikisha leo, tusilalamike kesho. Serikali imeleta huduma karibu, sisi tuitumie vizuri," alisema Lembris.
Kwa upande wake, Mshana Ndosi aliwataka Watanzania kupuuza maneno ya kuchochea chuki yanayozagaa mitandaoni na badala yake wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na hatimaye kupiga kura siku ya uchaguzi.
"Kura ni silaha yetu ya amani. Mimi nimeshaandikishwa leo hapa Geza Ulole, na nimefurahishwa na utaratibu mzuri ulioandaliwa na serikali yetu," alisema kwa furaha Mzee Ndosi.
Wananchi wengi waliofika kituoni hapo walionekana kuwa na nia ya dhati ya kushiriki uchaguzi ujao kwa amani na utulivu, wakisisitiza kuwa ni wajibu wa kila raia kulinda demokrasia na kuimarisha maendeleo ya nchi kwa kutumia sanduku la kura.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai