Afisa Tawala wilaya ya Hai Mary Mnyawi akimwakilisha mkuu wa wilaya ya Hai Juma Irando kwenye uzinduzi wa wiki ya sheria, amewataka wananchi kujitokeza kupatiwa msaada wa kisheria ikiwemo kujengewa uwezo wa njia bora za usuluhishi wa mogogoro.
Mnyawi amesema hayo Januari 23, 2023 katika uzinduzi huo ambapo kabla ya kutoa hotuba yake katika mahakama ya mwanzo Bomang'ombe, aliwaongoza wananchi na wadau wa sheria katika maandamano ya amani yaliyoanzia katika mahakama ya wilaya hiyo hadi mahakama ya mwanzo Bomang'ombe.
Aidha amewataka mahakimu na wadau wa mahakama kwa ujumla kutambua nafasi zao katika kutoa haki kwa wananchi endapo kutatokea kesi au utatuzi wa mogogoro.
Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Hai Julieth Mawole akizungumza katika uzinduzi huo ameeleza kuwa siku za hivi karibuni kumeibuka ukatili dhidi ya watoto ikiwemo ubakaji na ulawiti.
Hivyo wamejipanga kikamilifu kutoa elimu kwa watoto na jamii kwa ujumla kuhusu ubaya wa matukio hayo pamoja na adhabu ambazo sheria imeweka juu ya matukio hayo huku akiwataka wazazi kuwa karibu na watoto wao na kuwahoji maswali kuhusu maisha yao na miili yao kwa ujumla.
Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Hai Josia Gunda alipozungumza katika uzinduzi huo ameeleza kuwa taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa iko mbioni kuanzisha mfumo mpya wa mapambano dhidi ya rushwa kwenye ngazi ya kata (Takukuru Rafiki) kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya rushwa kuanzia ngazi ya kata ikiwa ni moja wapo ya njia ya kutatua matatizo kwenye jamii.
Awali akizungumza kwenye uzinduzi huo, diwani wa kata ya Bomang'ombe Evod Njau amewataka wananchi wa kata hiyo wenye kero na matatizo mbalimbali kutumia wiki ya sheria kutokeza kupeleka matatizo hayo kwenye jopo la mahakimu ili waweze kupatiwa msaada wa kisheria.
Kauli mbiu katika wiki ya sheria mwaka huu inaeleza "Umuhimu Wa Utatuzi Wa Mogogoro Kwa Njia Ya Usuluhishi Katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu Wa Mahakama Na Wadau"
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai