Wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai wametakiwa kuongeza ushiriki wao katika masuala yanayohusu utunzaji wa mazingira katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa na Afisa Mazingira wa Halmashauri hiyo Alfred Njegite akizungumza kwenye kipindi cha Siku Mpya kinachorushwa na Redio Boma wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Mazingira.
“Shughuli za utunzaji wa mazingira zinatakiwa kufanywa na kila mwananchi kwani kila mahali kwenye watu panakuwa na uzalishaji wa taka. Serikali peke yake haiwezi kufanya kazi hiyo bali itafanikiwa kama wananchi watashiriki kwa sehemu yao” Ameongeza Njegite.
Amesema maadhimisho ya Siku ya Mazingira mwaka huu hayatafanyika kwa kukusanyika bali kwa kutekeleza shughuli za utunzaji wa mazingira ikiwemo kuotesha miti, kufanya usafi wa mazingira, kutembelea na kuimarisha utunzaji wa mazingira kwenye vyanzo vya maji.
Naye Afisa Maliasili Wilaya ya Hai Mbayani Mollel ameikumbusha jamii ya wilaya hiyo kuendelea kupanda miti na kutunza miti iliyopo kwenye maeneo yao huku akibainisha faida za kuwa na misitu ni pamoja na kupata mvua za uhakika, kutunza vyanzo vya maji, kupata matunda na kivuli pamoja na hewa safi.
Amesema katika jitihada za kutunza mazingira halmashauri inaendelea kupanda miti kwenye vyanzo vya maji, kwenye maeneo ya wazi, kwenye hifadhi za misitu pamoja na kugawa na kuhamasisha wananchi kuotesha miti kwenye maeneo wanayoishi.
Kwa upande wake Afisa Kilimo wa wilaya hiyo David Lekei amewataka wananchi kufanya shughuli za kilimo na ufugaji kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira kwa kupanda mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi, kufanya kilimo cha kubadilisha mazao kwa mzunguko wa mazao yenye mizizi mirefu na ile yenye miziz mifupi.
Aidha Lekei amewakumbusha wananchi kubadilika kutoka kilimo cha kutegemea mvua na badala yake kutumia kilimo cha umwagiliaji huku akiwaasa kutumia kwa uangalifu rasilimali maji.
Tarehe 05 Juni kila mwaka imetengwa na Umoja wa Mataifa kuwa Siku ya Mazingira duniani ambapo dunia nzima inajumuika pamoja kutambua umuhimu wa mazingira na kukumbushana namna bora ya kuimarisha utunzaji wake.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai