Wanawake wajasiriamali Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro wametakiwa kubuni miradi yenye tija na mwelekeo wa viwanda ili waweze kujiongezea tija katika uzalishaji na kuongeza wigo wa ajira kwa jamii inayowazunguka.
Hayo yamesemwa Machi 8, 2022 na katibu tawala wilaya ya Hai Upendo Wella ambaye alimuwakilisha mkuu wa wilaya hiyo Juma Said Irando katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo kwa wilaya ya Hai yamefanyika katika viwanja vya Snow View.
Upendo Wella amesema vikundi vingi vya wanawake havipo katika mrengo wa viwanda vidogo vidogo jambo linalowakosesha wanawake mapato huku akiwakumbusha kuendelea kuwatumia wataalamu waliopo ngazi ya Halmashauri ili kujiongezea ujuzi na wigo wa ufanyaji wa biashara.
Awali akizungumza katika maadhimisho hayo ya siku ya wanawake Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe alisema miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo maji pamoja na barabara inaendelea kutekelezwa huku akiwakumbusha kuendelea kuiamini serikali kwa utekelezaji mzuri wa miradi inayowagusa wananchi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Edmund Rutaraka akitoa taarifa fupi ya mwenendo wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo ndani ya wilaya, amesema asilimia kubwa ya miradi imeshatengewa fedha na ipo katika hatua za utekelezaji.
Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa maadhimisho hayo ya siku ya wanawake akiwemo Neema Kweka amesema asilimia kubwa ya wanawake wameondokana na dhana ambazo zilikuwa zikiwafunga na kushindwa kujikita katika shughuli za kimaendeleo huku akisema masuala ya usawa wa haki kwa wanawake yamekuwa ni kipaumbele katika jamii kwa sasa.
Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yanafanyika kila tarehe 8 marchi kila mwaka na kwa mwaka 2022 wilaya ya Hai yamefanyika katika viwanja vya Snow View mjini Bomang’ombe yakiongozwa na kaulimbiu isemayo “Kizazi cha haki na usawa kwa maendeleo endelevu, jitokeze kuhesabiwa”.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai