MKUU wa wilaya ya Hai Onesmo Buswelu amewataka wananchi wanaonufaidika fedha zinzotolewa na mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kwa ajili ya kunusuru kaya masikini kutumia sehemu ya fedha hizo na kujiunga na bima ya afya.
Akizungumza na wananchi wanaonufaika na mpango huo wakati wa zoezi uhawilishaji wa fedha katika kijiji cha Tindigani aliwataka kuhakikisha kuwa wanajiunga na Bima ya afya ili waweze kupata matibabu pindi wanapougua.
“Serikali imelenga kuboresha maisha ya wananchi wake, ni vyema ninyi mnaopata fedha za TASAF kuzitumia pia kwa kujikatia bima ya afya ambayo inawapa nafasi ya kutibiwa katika zahanati na vituo vya afya pamoja na hospitali ya wilaya kwa kupitia Bima hiyo ”amesema Buswelu.
“Unaweza ukaanza kutenga fedha kidogo kidogo kadiri unavyopata kwa kila awamu na hatimaye ukafanikiwa kupata fedha zitakokuwezesha kuwa na bima yako itakayokupa na nafasi wewe na familia yako kupata huduma kwa uhakika” amefafanua.
“Mtu anaweza kupata maradhi muda wowote bila kujali kama ana pesa ama la lakini akiwa na bima ya afya anao uhakika wa kupata matibabu wakati wowote” amesisitiza.
Akizungumzia baadhi ya wanufaika kutumia fedha hizo kwa kununua pombe amesema kuwa serikali haitasita kuwaondoa katika mpango kwani lengo la mpango huo ni kuhakikisha kuwa kila mmoja anabadili hali yake kiuchumi.
Kwa upande wake mtendaji wa kijiji hicho, Theodora Kessy amesema tangu mpango huo kuanzishwa umeleta mabadiliko makubwa kwani wanufaika wengi wameweza kuanzisha miradi midogo ikiwemo ufugaji wa kuku na mbuzi.
“Mpango huu umeboresha mahudhurio ya wanafunzi shuleni , pia umechangia mwitikio kwa wanawake wenye watoto wadogo kuhudhuria kiliniki kama inavyotakiwa” alisema.
Naye Diwani wa kata ya Kia, Yohana Laizer aliwasisitiza wanufaika wa fedha hizo kutozitumia kwa matumizi ya kawaida badala yake wajitahidi kuanzisha miradi midogo watakayoweza kuimudu ili kujikomboa kiuchumi na kufanikisha lengo kuu la mradi huo.
“Mradi huu ni wa mda na ipo siku utafikia mwisho hivyo basi ni vyema kila mmoja wetu aliyepata bahati ya kunufaika akatumia mradi huu kwa malengo ya kujiinua kiuchumi ili mradi utakapofikia mwisho uwe na kitu cha kukusaidia kupata mahitaji yako ya muhimu” amesema Diwani huyo.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai