Serikali katika Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro imekabidhi pikipiki 15 kwa waratibu elimu kata ili kuwarahisishia usafiri wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Akikabidhi pikipiki kwa waratibu hao Katibu Tawala Wilaya ya Hai Upendo Wella amewataka waratibu kutumia vyombo hivyo vya usafiri kutekeleza majukumu husika ili kuleta matokeo chanya na kuinua elimu katika kata wanazozisimamia.
“Vitendea kazi mlivyopokea leo ni vya thamani kubwa kwa jumla na kwa moja moja hivyo nawataka mkavitunze ili viweze kutumika kutekeleza kazi iliyokusudiwa ya kutokomeza kabisa tatizo la wanafunzi kushindwa kusoma, kuandika na kuhesabu” amesema Wella.
Akizungumza kwenye zoezi hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo ameishukuru Serikali kwa kutambua uhitaji uliopo na kuamua kutoa vyombo hivyo vya usafiri kusaidia waratibu elimu kata kuyafikia maeneo ya kazi kwa urahisi.
Awali akisoma taarifa kwa mgeni rasmi; Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Hai Deograsia Mapunda amesema zimepokelewa pikipiki 15 zenye thamani ya shilingi za kitanzania millioni 45.
Pikipiki hizo zimetolewa na Wizara ya Elimu kupitia mradi wa kukuza stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (LANES) ikiwa ni utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli la kuhakikisha elimu inayotolewa nchini inakuwa bora na yenye kuleta matokeo chanya.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai