Katika msimu huu wa mvua za vuli ambazo zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali, wananchi wilayani Hai wameshauriwa kuendelea kupanda miti katika maeneo yao ili kuepukana na changamoto za kimazingira zinazoikabili dunia kwa sasa.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Afisa misitu katika Wilaya ya Hai Badi Hatibu aliposhiriki zoezi la kupanda miti katika tindiga la Boloti na kusema kuwa bado jitihada kubwa zinahitajika kwa wananchi kutambua umuhimu wa upandaji miti ambao utarejesha uoto wa asili ulioharibiwa na shughuli za kibinadamu.
Hatibu amesema kuwa shughuli za kibinadamu katika maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo eneo oevu la Boloti bado zimeendelea kuathiri uoto wa asili na kuleta changamoto kubwa za uhifadhi wa mazingira huku akidai kuwa uharibifu huo umekuwa na madhara ya moja kwa moja kadiri siku zinavyosonga.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la Floresta Tanzania ambalo ni moja ya wadau wa mazingira mkoa wa Kilimanjaro Richard Mhina amesema kuwa wananchi wanapaswa kuona umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kwa faida yao binafsi.
Mhina amesikitishwa na kitendo cha uharibifu unaoendelea katika eneo oevu la tindiga la Boloti lililohifadhiwa ambapo amesema kuwa wameshirikiana mara nyingi na ofisi ya misitu wilaya kupanda miti katika eneo hilo huku changamoto kubwa ikiwa ni uhifadhi wa miti hiyo ambapo mifugo wamekuwa wakiingia na kuiharibu kila wakati.
Kwa upande wake Kundankira Kimaro mkazi wa Kijiji cha Kware ameziomba serikali za vijiji vinavyozunguka eneo hilo kuona kuwa inao wajibu wa kuchukua hatua kali ili kulinda eneo ambalo yeye ameeleza kuwa endapo litatumiwa vyema litakuwa na tija kwa jamii kubwa.
Ikumbukwe kuwa eneo la Boloti lilitengwa na serikali kama eneo oevu japo kwa sasa linakumbwa na changamoto lukuki ikiwemo kuendelea kwa shughuli za kibinadamu ndani ya eneo hilo huku mamlaka husika zikifumbia macho bila kuchukua hatua zozote.
Kwa mujibu pia wa taarifa kutoka ofisi ya misitu wilaya zinaonesha kuwa ni zaidi ya mara nne wanapanda miti katika eneo hilo bila mafanikio katika uhifadhi na kwa wiki hii pekee miti zaidi ya elfu nane imepandwa kwa mara nyingine na swali kubwa likiwa ni Je endapo miti hiyo italindwa ama la.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai