Watanzania wametakiwa kuiunga mkono serikali katika juhudi zake za kuwaletea maendeleo kwenye maeneo yao kwa kushiriki kulipa kodi mbalimbali zilizowekwa kisheria huku wakitambua kuwa kodi ni msingi wa maendeleo ya nchi hasa kwa wakati huu ambapo nchi inajizatiti kuelekea uchumi wa wa kati kwa kuimarisha viwanda.
Wito huo umetolewa mapema leo Mei 23 na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Dk. Hasani Abass kwenye mahojiano na kituo cha Redio Boma Hai cha Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya kuwatembelea maafisa Habari na Mawasiliano wa Sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa.
Amesema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Magufuli imejizatiti kuwahudumia na kuwatumikia wananchi wake kwa kutatua changamoto mbalimbali za wananchi katika maswala ya maji, umeme pamoja na kufufua viwanda vidogo na vikubwa kwa lengo kuu la kuboresha maisha ya Mtanzania mmojammoja nan chi nzima kwa ujumla.
“Niwaombe wananchi waendelee kuiunga mkono serikali yao kuanzia viongozi waliopo kwenye ngazi ya wilaya yaani Mkuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Wabunge, Madiwani nikiamini kuwa viongozi wote hawa wana dhamira ileile ya Mhe. Rais ya kuona mtanzania anaondokana na kero ambazo hazina msingi wala hazina sababu ya kuwepo lakini pia viongozi waliopo niwaase waendelee kutekeleza kazi zao kwa kasi kama ambavyo Mhe. Rais anataka ili wananchi waweze kuona matokeo chanya”. Ameongeza Dkt. Abbas.
Aidha Dkt. Abbas amewataka wananchi kufuatilia kwa karibu utendaji wa serikali ya awamu ya tano na kujionea hatua zinazopigwa katika kuleta maendeleo ya nchi kwani kwenye kila sekta kuna kazi kubwa ya kimageuzi inafanyika huku akitolea mfano sekta ya nishati inayoboreshwa kwa utekelezaji wa miradi ya Kinyerezi I ambayo upanuzi wake ukikamilika utazalisha megawati za umeme 185; mradi wa Kinyerezi II utakaozalisha megawati 240 umeshazinduliwa pamoja na mradi mkubwa wa Stigler’s Gorge ambao ni mradi wa kihistoria utakaozalisha megawati 2100 za umeme ukiwa kwenye hatua ya uchambuzi baada ya kutangaza zabuni.
Pamoja na miradi mingine, Dkt. Abbas amezungumzia utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa itakayounganisha Tanzania na nchi jirani ya Rwanda ambayo itaanzia Daresalam huku akibainisha kuwa treni hizo zitaendeshwa kwa umeme huku serikali ikipiga hatua nyingine kubwa ya kutangaza zabuni ya kuleta mabehewa na vichwa vya treni 1590 ambapo kati yake mabehewa 1560 yatakuwa ya kubeba mizigo ya aina mbalimbali na yaliyobaki yatakuwa ya kubeba abiria.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO) Paschal Shelutete amewakumbusha maafisa habari wa Halmashauri jukumu lao kuu la kuwahabarisha wananchi kuhusu maswala ya maendeleo na kuwataka wasiwe kikwazo cha utoaji taarifa kwa wananchi bali wao wawe chachu ya kufanikisha taarifa kuwafikia wananchi kuhusiana na utekelezaji wa kazi za serikali katika maeneo yao kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wametekeleza vizuri jukumu lao la kumsaidia Mhe. Rais katika juhudi za kuleta maendeleo nchini.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai