Wito umetolewa kwa watumishi wa umma kutimiza wajibu na majukumu ya kazi zao kwa uadilifu na kuimarisha huduma kwa wananchi walio kwenye maeneo yao.
Akizungumza kwenye ukumbi wa Halmashaur ya Wilaya ya Hai wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha maafisa watendaji wa Halmashauri hiyo; Simon Msoka Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji) akimuwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro.
Msoka amesema watendaji wa vijiji, kata na maafisa tarafa ndio kiungo kikubwa cha kuwahudumia wananchi na kwamba ndio wanaofahamu mahitaji halisi ya wananchi kwenye maeneo yao kwani ndio waliopo karibu nao.
Aidha amewataka watendaji hao kuhakikisha wanatatua kero za wananchi kwenye maeneo yao ili kupunguza na hatimaye kuondoa malalamiko yanayopelekwa na wananchi kwa viongozi wa kitaifa.
“Ni jambo la aibu kuona wananchi wanapeleka malalamiko yao kwa viongozi wa kitaifa; hii inaonesha kuwa wapo watendaji wa vijiji, kata na maafisa tarafa walioshindwa kutimiza wajibu wao”. Amesema Msoka.
“Ukikuta wananchi wengi wamejaa kwenye ofisi ya Mkurugenzi au Mkuu wa Wilaya ni lazima wewe kama mtendaji wa kijiji ujiulize kama kweli unatosha kwenye nafasi yako” Amesisitiza.
Aidha Msoka amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai kuweka mazingira ya kutoa elimu ya mara kwa mara kwa watumishi wa kada mbalimbali hasa kundi la Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na Watendaji wa Vijiji kupatika mafunzo ya namna hii kila mwaka.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amemwakikishia Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro kuwa halmashauri yake ipo tayari kusimamia maelekezo yaliyotolewa kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo.
Sintoo amesema kuwa ofisi yake itahakikisha watumishi wanatekeleza wajibu wa majukumu yao kwa ufanisi unaotakiwa ikiwa ni juhudi za kuunga mkono kazi nzuri inayofanywa na serikali kuu yenye lengo kuu la kuboresha huduma kwa wananchi.
Halmashauri ya Wilaya ya Hai inaendesha Kikao Kazi kwa Maafisa Tarafa, Maafisa Watendaji wa Kata na Maafisa Watendaji wa Vijiji vyote vya halmashauri hiyo ambacho kinalengo la kuboresha utendaji wao wa kazi, kuimarisha huduma kwa wananchi na kuwapatia uelewa wa mambo mtambuka yanayohusu jamii wanazozihudumia pamoja na jamii za taasisi na mashirika yanayotoa huduma kwenye maeneo yao.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai