Wito umetolewa kwa wananchi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mfumo wa umeme kwenye majengo yao hasa nyumba za makazi na ofisi ili kuepuka majanga ya moto yanayosababishwa na hitilafu kwenye mifumo hiyo.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Mafunzo wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Kilimanjaro Sajenti Elias Manyama wakati wa mafunzo ya namna ya kukabiliana na majanga ya moto kwa watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Hai.
Amesema kuwa ni jambo la msingi kufanya ukaguzi wa mfumo wa umeme wa jengo ili kubaini hitilafu kabla hazijaleta madhara huku akisisitiza kuwa kila jengo linatakiwa kufumuliwa na kuwekwa mfumo mpya kila baada ya miaka 15.
Manyama amesema kuwa chanzo kikuu cha moto ni mwanadamu mwenyewe na namna anavyoendesha maisha yake kwa kufanya uzembe wakati wa kutumia vifaa vyenye kusababisha moto kama gesi za kupikia, matumizi ya vifaa vya umeme na mengineyo.
Aidha Manyama amewataka wananchi kujenga mazoea ya kuwa na vifaa vya kuzimia moto kwenye maeneo yao ya kazi na makazi pamoja na vyombo vya usafiri ili kuwa kwenye nafasi nzuri kudhibiti moto iwapo utatokea.
Katika kuwaongezea ufahamu kuhusu aina za moto na namna ya kudhibiti; Manyama amesema kuna moto aina A unaohusu viti vitokanavyo na mimea kama majani, kuni, mkaa na nguo ambavyo huzimwa kwa kutumia maji au kizimia moto cha mapovu.
Aina nyingine ni moto kundi B wa mafuta ambao huzimwa kwa kutumia kizimia moto cha poda, moto kundi C unahusisha aina mbalimbali za gesi ambao huzimwa kwa kutumia kizimia moto cha poda au cha hewa ya kaboni. Moto kundi D ni moto wa vyuma ambao huzimwa kwa kizimia moto cha poda pamoja na aina nyingine ya moto kundi E unaohusu vifaa vya umeme kama transifoma, kompyuta na vingine unaoweza kuzimwa kwa kutumia kizimia moto cha poda.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai