Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Yohana Sintoo ameongoza watumishi wa makao makuu ya halmashauri hiyo kuhamasisha unywaji wa maziwa kwa jamii.
Akizungumza kwenye kikao cha asubuhi na watumishi hao Sintoo amewataka watumishi na wananchi kwa ujumla kujizoesha tabia ya kunywa maziwa kwani maziwa yana faida nyingi kwenye mwili wa binadamu.
Mkurugenzi Mtendaji amewahamasisha watumishi kunywa maziwa na kuwakumbusha kuwa wanatakiwa kuwa mabalozi wa mambo mazuri yenye faida kwa jamii na kwa kusisitiz hili Sintoo amewanunulia watumishi wote wa makao makuu kikombe kimoja cha maziwa kama motisha wa kuhamasisha wengine.
“Leo natoa ofa kwa watumishi wote wa makao makuu kunywa glasi moja ya maziwa ili kuwahamaisha na ninyi mkanunulie famila zenu, marafiki na majirani zenu ili kuambukizana tabia njema ya kunywa maziwa” Ameongeza Sintoo.
Sintoo amefikia kutoa rai hiyo baada ya kupokea taarifa za Idara ya Mifugo na Uvuvi iliyowasilishwa na Mkuu wa Idara hiyo Elia Machange ya uwepo wa mashine ya kielektroniki ya kuuzia maziwa (ATM ya Maziwa) katika Wilaya ya Hai.
Machange amesema kuwa ATM hizo zimegawiwa kwa kikundi cha vijana wa Nronga Wilaya ya Hai ambao walishindanishwa na vikundi vingine 20 vya vijana wanaojishughulisha na biashara ya maziwa katika wilaya za Hai na Siha.
Akizungumzia mashine hiyo Mkani Waziri ambaye ni Mshauri Mwelekezi na Meneja Mradi Tanzania wa kampuni ya Match Maker amesema mashine hizo zenye thamani ya shilingi milioni 16.5 (Tshs.16,500,000) zimepatikana kupitia mradi wa Dairy Profit unaotekelezwa kwenye nchi tatu za Uganda, Kenya na Tanzania unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya.
Kwa upande mwingine Vickyneema Dickson mmoja wa vijana wa mradi wa maziwa Nronga amesema kuwa ATM hiyo ya maziwa inawawezesha wateja kununua maziwa kulingana na uwezo wao kuanzia sh. 500 na kuendelea na kwamba huduma hiyo inapatikana kila siku kuanzia saa moja asubuhi hadi saa tatu usiku.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Hai Dkt. Emmanuela Urassa amesema kunywa maziwa kuna faida nyingi kwa mwanadamu ikiwemo kupata madini ya Calcium yanayoimarisha meno na mifupa, pia kuna protini inayompa mtu nguvu, fosforasi inayosaidia kutengeneza nguvu na kuimarisha mifupa ikiwemo na Vitamini B12 inayosaidia utengenezaji wa chembechembe nyekundu za damu, na kusaidia mishipa ya fahamu ifanye kazi kwa ufanisi.
"Inashauriwa mtu anywe glasi moja ya maziwa kila siku ili apate manufaa na faida nilizotaja kwenye meno, mifupa na kwenye mishipa ya fahamu". Amesema Dk. Urassa.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai