Watumishi Wampongeza DC Ushiriki Kuboresha Huduma za Afya
Imetumwa: February 12th, 2021
Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya amewashukuru kwa zawadi aliyopewa na watumishi wa Idara ya Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Hai kwa kutambua mchango wake katika kazi wanazofanya huku akisisitiza kuwa lengo kuu ni kuwapunguzia wananchi changamoto wanazokutana nazo.
Sabaya amesema ni jambo jema kwa kutambua mchango wa mtu kwenye jamii kwa sababu inatia moyo kwa anayetambuliwa lakini pia inaamsha ari ya kujituma na kufanya kazi kwa bidii akiamini kuwa utamaduni huo utasaidia kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi katika ngazi zote.
Sabaya ameshiriki kikamilifu katika kuibua wazo la kujenga kituo cha afya cha kisasa kwenye ukanda wa tambarare wa wilaya ya Hai na kuvishirikisha vyama vya ushirika vilivyopo kwenye wilaya hiyo hatimaye kufanikiwa kupatikana fedha kiasi cha shilingi milioni 38 zinazotumika kujenga kituo cha afya cha Longoi.
Aidha Sabaya ametoa wazo la kuanzishwa au kuimarishwa huduma kadhaa katika vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo hospitali ya wilaya ya Hai. Mojawapo wa huduma hizo ikiwa ni kitengo cha huduma za kinywa na meno iliyozinduliwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. David Silinde.
Imefahamika kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo amekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha utendaji kazi wa Idara ya Afya kupitia hospitali ya wilaya pamoja na vituo vya kutolea huduma kwenye wilaya hiyo hadi kupelekea watumishi hao wakiongozwa na Mganga Mkuu wa halmashauri hiyo Dkt. Irene Haule kukabidhi zawadi hiyo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt. Irine Haule amesema kuwa Mkuu wa wilaya huyo amekuwa mara kwa mara akitoa ushauri wa namna bora ya kutekeleza kazi mbalimbali zinazohusu huduma za afya kwenye wilaya hiyo ikiwemo kutatua migogoro mbalimbali inayojitokeza.
“Mara kwa mara Mkuu wa Wilaya amekuwa msaada kwetu katika kutekeleza kazi zetu hasa pale tunapokutana na changamoto za kimaamuzi; mfano wa karibu ni ushiriki wake wakati wa kuandaa mpango wa bajeti ya afya kwa mwaka wa fedha 2021/2022” Amesema Dkt. Haule.
Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo wakiwemo Katibu Tawala Upendo Wella na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Yohana Sintoo wamekuwa chachu ya maendeleo katika halmashauri hiyo katika sekta mbalimbali kama afya, elimu, maji, nishati na nyingine katika kuboresha maisha ya wananchi katika wilaya hiyo.