Serikali katika wilaya Hai mkoani Kilimanjaro imedhamiria kusimamia na kutekeleza kikamilifu sheria ya makosa ya jinai kwa mtu atakayejihusisha na masuala ya ukatili kwa watoto.
Hayo yamebainishwa na Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Hai Helga Simon wakati wa mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo wanajamii wa vikundi vya kiuchumi ili kuiongezea jamii ufahamu wa vitendo vya ukatili.
Amebainisha kuwa serikali haina mchezo kwenye ulinzi wa watoto huku akisema kuwa mtu yeyeote atakayehusika kumtoa ujauzito mwanafunzi ili kupoteza ushahidi atawajibishwa kwa mujibu wa sheria za makosa ya jinai ili kupunguza wimbi la wazazi au walezi kushiriki makossa hayo.
“Tumeamua kushirikisha jamii ili elimu ya masuala ya ukatili ienee kwenye jamii ili kuongeza wigo wa kupambana na masuala hayo kwani wanajamii wanafahamiana na wanaishi pamoja kwenye maeneo yao” Amesema Helga.
Aidha Helga ametoa wito kwa wanajamii kuwajibika kila mmoja kwenye eneo lake kama mzazi, mlezi, jirani au kiongozi wa kijamii kwa kutoa taarifa za vitendo vya ukatili vinavyofanyika kwenye maeneo yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto la Polisi Wilaya ya Hai Happiness eliufoo amesema kuwa wanaendelea kusimamia sheria zilizowekwa na kwamba mtu yeyeote atakayepatikana kutenda kosa la ukatili ikiwemo kuwatoa mimba wanafunzi atafikishwa mbele ya vyombo husika.
“Wilaya ya Hai bado ipo kwenye mapambano ya kutokomeza vitendo hivi vya ukatili. Tunatumia njia mbalimbali kuelimisha jamii kwenye mikutano na pia kwa kutumia redio Boma FM ili kuwafikia wananchi wengi Zaidi na hatimaye kuwa na jamii inayotambua na kupiga vita aina zote za ukatili” Amesema Eliufoo.
Naye Mathayo Mlay amesema amefurahia mafunzo waliyopatiwa kwani yamemsaidia kupata uelewa wa masuala yanayohusu ukatili hivyo kuwafanya waweze kushiriki katika vita ya kupambana na vitendo hivyo.
Vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa watoto vimekuwa vikichangia kuharibu ndoto za watoto ambao ni tengemeo la Taifa na kusababisha kupunguza nguvu kazi huku maafisa ustawi wa jamii na dawati la jinsia na watoto wakiwekeza nguvu kubwa kupambana na vitendo hivyo.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai