Wilaya ya Hai Kutoa Chanjo kwa Watoto 42,000 Kuwakinga Magonjwa
Imetumwa: May 10th, 2021
Jumla ya watoto 42,253 wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wanatarajia kupatiwa chanjo ya ugonjwa wa kichocho na minyoo Mei 17, 2021 kwa lengo la kudhibiti magonjwa hayo yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.
Akifungua kikao cha mpango mkakati wa kudhibiti magonjwa hayo Afisa Tawala wilaya ya Hai Marry Mnyawi ambaye amemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya, amewataka washiriki wa kikao hicho ambao ni wakuu wa idara na wajumbe mbalimbali kutoka halmashauri kuwa mabalozi wazuri katika kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo hiyo.
“Kufuatia kikao hiki cha mpango mkakati ninaamini tutakwenda kuwa mabalozi wazuri kuelimisha wenzetu na kuwaelekeza wananchi wanaotuzunguka kuhusu umuhimu wa chanjo hii ili kuepuka taarifa za mtaani ambazo si sahihi na za upotoshaji kwamba chanjo hizi zina madhara” amesema Mnyawi.
Aidha ameeleza kwamba Serikali imekuwa ikiweka mkakati kila mwaka wa kuhakikisha kuwa zoezi la utoaji wa chanjo linaendeshwa kikamilifu ili kila mtoto aweze kupatiwa chanjo hiyo.
Kwa upande wake mratibu wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele wilayani humo Dkt. Apolnary Tesha amefafanua kuwa zoezi la utoaji wa chanjo hiyo limekuwa likiendeshwa kwa mwaka wa tano mfululizo hadi sasa katika wilaya ya Hai na kuongeza kuwa hakuna athari yoyote mbaya iliyowahi kujitokeza kwa watoto wanaopatiwa chanjo hiyo.
“Ninachoweza kuiasa jamii ni kwamba dawa hizi ni salama na kwa wilaya ya Hai dawa hizi za chanjo tumezitoa kwa mwaka wa tano sasa na hatujawahi kupata madhara yoyote kwa hiyo nawahakikishia wazazi na walezi waendelee kuzitumia dawa hizi kwa ajili ya kujikinga na haya magonjwa ambayo ni hatari kwa maisha yetu” Amesema Dkt. Tesha.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa shule za msingi wilaya ya Hai Christopher Wangwe akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo ameeleza utaratibu uliowekwa kwa shule zote 130 kwa ajili ya kuwapatia wanafunzi chanjo hiyo.
Wangwe amesema kuwa amewaelekeza walimu wakuu wa shule hizo kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapatiwa chakula mapema ili kupata muda wa kukamilisha zoezi hilo kwa ufanisi.
Inakadiriwa kuwa watu bilioni 1 duniani kote wameathiriwa na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ambapo nchini Tanzania wananchi wote wapo hatarini kuambukizwa magonjwa hayo.