Wananchi wa kata 8 za wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wanajiandaa kupokea mradi mkubwa wa maji utakaowaondolea adha ya kukosa maji iliyowakabili kwa muda mrefu .
Akifungua kikao kazi cha mafunzo kwa wakulima yenye lengo la kutoa elimu ya tathmini ya udongo katika wilaya ya Hai, mbunge wa jimbo hilo Saashisha Mafuwe amesema kuwa visima 18 vimeanza kuchimbwa chini ya mamlaka ya maji mkoa wa Arusha vitakavyosaidia kutokomeza kero ya maji jimboni humo.
Saashisha amebainisha kuwa tayari wameandaa mtandao wa mahitaji ya maji ndani ya jimbo hilo kwa kuanza na wakazi wa kata 8 zilizopo eneo la tambarare ambazo ni Kia, Bomang'ombe, Muungano, Masama Kusini, Weruweru, Mnadani na Bondeni.
Akizungumzia Sera yake ya kilimo na viwanda katika jimbo la Hai, mbunge huyo ameeleza kuwa kusudi la serikali ni kuhakikisha kuwa kila mkulima analima kilimo chenye tija ikiwa ni pamoja na namna ya kuyaongezea thamani mazao kabla ya kuyapeleka sokoni.
Kwa upande wake Afisa kilimo wa wilaya ya Hai David Lekei amesema kuwa uchumi wa taifa lolote duniani unachochewa na kilimo hivyo wameendelea kutoa elimu kwa wananchi namna ya kulima kilimo chenye tija ikihusisha pia mazao ya kimkakati ikiwa ni pamoja na Kahawa, Vanilla na Migomba.
Naye afisa kutoka kituo cha utafiti wa kahawa (TACRI) Tesha amewahimiza wakulima wa mazao ya kimkakati ikiwemo kahawa kupanda miche bora na ya kisasa iliyofanyiwa utafiti na kituo hicho kwa lengo la kupata mazao mengi
Kikao hicho ambacho kimerushwa moja kwa moja na redio Boma Hai fm kimehusisha maafisa mbalimbali akiwemo mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Hai Yohana Sintoo, wakuu wa idara, na taasisi mbalimbali za utafiti wa udongo na zana za kilimo.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai